Kila kona Ulaya ni Samagoal

Muktasari:

  • Msimu huu wa 2018/2019, Samatta ameifungia KRC Genk mabao 25 katika mashindano yote aliyocheza, tisa yakiwa  ya Europa Ligi na 16 Jupiler Pro. 

Dar es Salaam. Acha Neil Warnock anaendelea kutafuta tiba katika usajili wa dirisha dogo mwezi huu, macho yake yametua kwenye klabu mbalimbali Ulaya.

Mmoja wa watu anayemtolea macho ni mshambuliaji nyota na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta anayecheza katika kikosi cha KRC Genk ya Ubelgiji.

Acha wazungu wapagawe. Acha wazungu wamtungie wimbo...Sama…Sama...Sama....Goal maana mambo anayofanya huko si ya kawaida.

Huyu ni mtoto wa Mbagala Market FC iliyomuibua ambaye leo hii akikatiza mitaa ya Brussels kule Ubelgiji wanatambua shughuli anayoifanya uwanjani.

Hiyo ndiyo iliyosababisha pia makocha mbalimbali akiwemo kocha Neil Warnock wa Cardiff kuendelea kutafuta tiba katika usajili wa dirisha dogo mwezi huu, macho yake yametua kwenye klabu mbalimbali Ulaya ikiwemo kutupia jicho kwa mshambuliaji huyo nyota na nahodha wa Taifa Stars, anachezea kikosi cha KRC Genk ya Ubelgiji.

Samatta siyo mchezaji maarufu sana Ulaya kama akina Kylian Mbappe wa PSG au Marcus Rashford wa Manchester United, lakini kwanini kocha huyo wa Cardiff anamtaka kwa udi na uvumba. Hakuna jambo la ziada ambalo Cardiff inataka kutoka kwa Samatta zaidi ya mabao tu. Mabao ndiyo jibu sahihi analoweza kukupa Warnock.

Kocha huyo anasema Samatta ni mchezaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao na siku zote angependa kuwa naye katika kikosi chake. Samatta ni mchezaji anayetarajiwa kucheza muda mrefu kutokana na umri wake wa miaka 26 unaotoa fursa kwake kucheza muda mrefu. Magazeti ya Ulaya yanamtaja Samatta ni mshambuliaji asilia mwenye kasi na uwezo wa kulifuata lango akitaka kutimiza kazi yake ya kufunga mabao.

Msimu huu wa 2018/2019, Samatta ameifungia KRC Genk mabao 25 katika mashindano yote aliyocheza,  tisa yakiwa  ya Kombe la Europa na 16 Jupiler Pro.  Mapema wiki hii mshambuliaji huyo alitia saini mkataba mpya na klabu yake baada ya kukataa ofa lukuki zilizowasilishwa mezani kwao katika usajili wa dirisha dogo.

Huu ni msimu wa nne kwa mshambuliaji huyo kucheza soka la kulipwa Ubelgiji, msimu wake wa kwanza ilikuwa ni 2015/16 ambapo alifunga mabao matano katika michezo 18 ya Jupiler Pro. Spoti Mikiki inakuletea klabu ambazo nyota huyo ameziingiza vitani kuwania saini yake kipindi hiki cha usajili wa dirisha dogo   zikiwemo Everton na West Ham United za Ligi Kuu England.

Everton Tangu aondoke Romelu Lukaku mwaka 2017, mahasimu hao wa Liverpool, Everton imekuwa na changamoto kwenye safu yao ya ushambuliaji.

Wamekosa aina ya mtu kama Lukaku aliyekuwa na uwezo wa kufunga zaidi ya mabao 15 katika kila msimu, Julai 9, 2017  waliamua kumrejesha nyota wao wa zamani,  Wayne Rooney  lakini kwa bahati mbaya hakuwa  tiba.

Kutokana na tatizo hilo ambalo linaendelea kuisumbua Everton, kocha wa timu hiyo, Marco Silva ameonyesha nia ya kumuhitaji Samatta ili kuongeza nguvu katika kikosi chake.

Imekuwa ikimlazimu Silva kumtumia mara kadhaa Mbrazil Richarlison kama namba tisa licha ya kuwa kiasili ni winga. Nyota huyo wa zamani wa Watford ameifungia Everton mabao tisa katika michezo 20.

West Ham United

‘Wagonga nyundo’ wa London, West Ham United wameingia katika mtego huo na kuwa miongoni mwa timu zinazotaka huduma ya Samatta ambaye amewahi kuwa mchezaji bora kwa wachezaji wa ndani Afrika kabla ya kutimkia Ulaya.

Cardiff City

Samatta, ameingia katika rada za timu ya Cardiff inayoshiriki Ligi Kuu England ambao wanataka kuweka mezani pauni milioni 13 (sawa na Sh38 bilioni) kumsajili katika dirisha hili dogo. Hata hivyo, KRC Genk imegomea ofa hiyo, hivyo itawalazimu Cardiff kuongeza kitita cha fedha ili kumnasa mshambuliaji huyo ambaye hivi karibuni aliongeza mkataba wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo.

Schalke O4

Wababe hao wa Ujerumani waliingia kwenye vita ya Samatta wakiwa na Borussia Dortmund,  Werder Bremen na VfB Stuttgart pamoja na uwepo wa timu hizo nyingine wanaopewa nafasi kubwa ya kumsajili mshambuliaji huyo ni Schalke O4.

Fenerbahce

Vyombo vya habari ya Uturuki viliripoti kuwa jina la Samatta limependekezwa na kocha wa timu hiyo,  Ersun Yanal kipindi hiki cha usajili kama mchezaji anayeweza kutatua changamoto waliyonayo kwenye safu yao ya ushambuliaji. pamoja na uwepo wa majina makubwa kama Roberto Soldado aliwahi kuichezea Tottenham na Andrew Ayew ambaye naye anakumbukwa kwa kuwika na Swansea City zote zikiwa za England wameshindwa kuifanya  Fenerbahçe kuwa na makali kwenye safu ya ushambuliaji. Yanal kwenye moja ya mikutano yake na waandishi wa habari ya hivi karibuni alinukuliwa akisema anauhitaji mkubwa wa kuongeza mshambuliaji mwingine kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili kama itashindikana itamlazimu suburi hadi majira ya kiangazi.

Burnley na Brighton

Ukiachilia mbali Everton na West Ham United, Burnley pamoja na Brighton & Hove Albion nao wameingia katika vita hiyo ya kutaka huduma ya Samatta aliyewahi kuzitumikia African Lyon, Simba kabla ya kujiunga na TP Mazembe Englebert ya DR Congo.