VIDEO -Kikwete kunogesha harambee Yanga

Muktasari:

  • Fedha hizo zinakusanywa katika kampeni iliyoanzishwa na kocha mkuu wa timu hiyo Mkongoman, Mwinyi Zahera ya kuichangia Yanga kwa mashabiki wake kupitia benki na mitandao ya simu za mkononi.

Dar es Salaam. Rais wa awamu ya nne ya Tanzania, Jakaya Kikwete atawaongoza wanachama na mashabiki wa klabu ya Yanga katika Tamasha la Kubwa Kuliko lenye lengo kuchangishana Sh1.5bilioni kwa klabu hiyo.

Akizungumza katika mahojiano maalumu leo makao makuu ya Ofisi za Mwananchi, Tabata Relini, Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Kamati ndogo ya uhamasishaji ya Yanga, Dk David Ruhago alisema wageni mbalimbali wamealikwa kushiriki katika harambee hiyo.

"Rais Kikwete amethibitisha kuwepo siku hiyo, lakini pia tunatarajia mgeni rasmi awe mtu mkubwa nchini, wazee wa klabu yetu, wachezaji wa zamani pia watakuwepo" alisema Dk Ruhago.

Alisema lengo ni kukusanya Sh 1.5 Bilioni na siku hiyo kazi waliyopewa ya kukusanya michango ya klabu itahitimishwa.

"Suala ni kiasi gani hadi sasa tumekusanya naomba tupewe muda tutalizungumza hapo baadaye, lakini matarajio yetu yalikuwa ni kukusanya Sh1.5bilioni mchakato umeenda vizuri na bado tunaendelea na uchangiuzaji."

"Kadi za kushiriki kwenye harambee yetu zimeanza kuuzwa katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam na kwenye mtandao," alisema.

Kadi hizo zinauzwa kwa Sh 50,000, 100,000, 1 Milioni, 5 Milioni na 10 Milioni kwa meza ya watu 10 ambao wataamua meza hiyo ipambwe vipi.

Akizungumzia faida ya michango hiyo, Dk Ruhago alisema kwanza imeleta amani na sasa mambo yanakwenda vizuri ndani ya klabu.

"Klabu ina amnaiu, mambo yanakwenda na wanachama wamehamasika kuichangia klabu yao jambo ambalo ni jema," alisema Dk Ruhago.