Kikwete afichua dawa AFCON

Muktasari:

Akifahamu fika kuwa mwishoni mwa wiki ijayo nchi hizo wanachama wa SADC zitakutana kwenye Mkutano Mkuu jumuiya hiyo utakaofanyika jijini Dar es Salaam, Kikwete ametoa ushauri ambao pengine ukifanyiwa kazi unaweza kuboresha hali ya soka kwa nchi hizo.

RAIS wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ni miongoni mwa watu ambao hawajafurahishwa na kufanya vibaya kwa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kwenye Fainali za Mataifa ya Afrika (Afco) zilizomalizika huko Misri mwezi uliopita.

Ukiondoa Stars, kumbe Rais Kikwete pia huwa hafurahii kuona nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika(SADC) ambazo Tanzania ni miongoni, zikinyanyasika mbele ya mataifa ya Kaskazini na Magharibi mwa Afrika kwenye mashindano mbalimbali ya soka barani humu.

Akifahamu fika kuwa mwishoni mwa wiki ijayo nchi hizo wanachama wa SADC zitakutana kwenye Mkutano Mkuu jumuiya hiyo utakaofanyika jijini Dar es Salaam, Kikwete ametoa ushauri ambao pengine ukifanyiwa kazi unaweza kuboresha hali ya soka kwa nchi hizo.

“Kwa sasa ni vigumu kuiweka ajenda hiyo kwenye mkutano wa SADC unaotarajiwa kufanyika hapa nchini, lakini lazima tufahamu kwamba michezo ni muhimu,” alisema Kikwete.

“Kwa maoni yangu nadhani nchi za SADC tunatakiwa kujadili kwamba kwa nini hatupo katika kundi la nchi zilizo na kiwango cha juu soka barani Afrika.

“Tunaweza kuunda kitu kinaitwa Pan SADC Initiative kwa ajili ya kukuza michezo na hasa soka.”

Wazo la Rais huyo mstaafu ambaye ni mpenzi wa michezo limekuja mwezi mmoja baada ya kumalizika kwa fainali za 32 za Afcon zilizofanyika nchini Misri kuanzia Juni 21 hadi Julai 19 ambapo Algeria ilitwaa ubingwa.

Licha ya SADC kuwakilishwa na nchi saba kwenye mashindano hayo ambazo ni Angola, DR Congo, Madagascar, Namibia, Afrika Kusini, Tanzania na Zimbabwe hakuna hata timu moja iliyofanikiwa kutinga hatua ya nusu fainali.

Kwa ujumla kwenye awamu ya 32 za mashindano ya Afcon, timu kutoka nchi wanachama wa SADC zimetwaa taji hilo mara nne tu ambazo ni DR Congo iliyotwaa mara mbili na Afrika Kusini, sambamba na Zambia ambazo kila moja imechukua ubingwa mara moja.