Kikoti, Bigirimana waitesa Namungo

Muktasari:

Mikataba ya Bigirimana na Lusajo inaisha Julai mwaka huu wakati Kikoti bado ana mkataba wa mwaka mmoja kuitumikia Namungo FC ambayo inashika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na pointi 50,

Dar es Salaam. Kocha Thierry Hitimana amesema kama nyota wake watatu, Reliants Lusajo, Blaise Bigirimana na Kikoti wataondoka kwenye kikosi cha Namungo kwenye usajili wa dirisha kubwa, ndipo atafikiria kusajili wachezaji wapya kwenye timu hiyo.

Kocha Hitimana ameeleza kuwa na taarifa za nyota hao kutakiwa na timu nyingine, hivyo endapo wataondoka kwenye dirisha kubwa ndipo atafanya usajili wa kuziba nafasi zao, la sivyo ataendelea na kikosi chake cha awali.

"Bado sijafikiria kuongeza wala kupunguza mchezaji, lakini ikitokea baadhi ya wachezaji wangu ambao nasikia wanatakiwa na timu nyingine wakaondoka, basi nitaongeza wachezaji wachache ili kuziba nafasi zao," alisema kocha Hitimana na kuendelea.

"Nimesikia Kikoti, Lusajo na Bigirimana wanaweza kuondoka kwa kuwa wanatakiwa na timu nyingine, ingawa bado haijawa uhakika, ila kama usajili wao kwenye hizo timu zinazowataka ukitiki, basi sitokuwa na namna,".

Nyota hao ambao wanaongoza kwenye msimamo wa wapachika mabao kwenye kikosi cha Namungo inasemekana kuwa wako kwenye rada za timu za Simba, Yanga na Azam FC.