Kikosi cha mashabiki Yanga chapotea njia

Muktasari:

Niyonzima, ambaye aliokosekana kwenye mchezo uliopita dhidi ya Tanzania Prisons kutokana na kusumbuliwa na malaria umuhimu wake ulionekana jana kutokana na kucheza vizuri eneo la kiungo, lakini timu haikupata matokeo.

KOCHA wa Yanga, Luc Eymael jana aliwafurahisha mashabiki wa timu hiyo kwa dakika kadhaa, lakini akaishia kupata hasara kwa timu yake kulazimishwa sare na Polisi Tanzania kwenye mechi ya Ligi Kuu iliyochezwa katika Uwanja wa Ushirika mjini Moshi.

Awali, mashabiki wa Yanga kuanzia uwanjani mpaka kwenye mitandao ya kijamii walikuwa wakilalamika juu ya baadhi ya wachezaji kutotumika ipasavyo huku wakiwataja kabisa kwa majina Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima na Tariq Seif.

Mashabiki walikuwa wakidai kwamba kwenye sare dhidi ya Prisons, Tariq hakuchezeshwa kwenye nafasi sahihi huku Nchimbi na Haruna Niyonzima wakiwekwa benchi na ndio sababu timu haikushinda na kushinikiza waanze dhidi ya Polisi.

Kwenye sare ya jana wachezaji hao watatu walichezeshwa kwenye nafasi zao halisi na kushuhudia Yanga ikiwa na uhai kipindi cha kwanza kwa kushambulia kwa nguvu na kupata bao kupitia kwa Tariq dakika ya 40. Krosi iliyochongwa na Nchimbi ilipanguliwa na kipa na kumkuta Morrison aliyetoa pasi kwa mfungaji huyo aliyekwamisha mpira wavuni kwa kichwa.

Lakini, baada ya hapo kibao kilibadilika mchezo ukabalansi huku bao moja la Polisi likikataliwa kwa madai kwamba mfungaji aliotea.

Eymael licha ya jana kugoma kuzungumza lakini hivi karibuni alinukuliwa akisema atachezesha kikosi na mastaa wanaotajwa na wanaolalamika ndio watakaoamua.

Hata hivyo, nahodha wa Yanga, Papy Tshishimbi alisisitiza kuwa: “nadhani kocha ameona upungufu atafanyia kazi, lakini hatukati tamaa, hii ni sehemu ya mchezo.”

Sixtus Sabilo alifunga bao la kusawazisha la wenyeji dakika ya 71 ya mchezo na kuibuka shujaa baada ya kutibua mipango ya Yanga ambayo makomandoo wao walionekana mjini Moshi tangu juzi kuweka mazingira sawa.

Katika mechi ya mwisho timu hizo zilipokutana Uwanja wa Taifa, Yanga iliambulia pointi moja pia baada ya kukubali sare ya mabao 3-3.

Pia mfungaji wa bao la Polisi jana, Sabilo, ameingia kwenye rekodi ya kuzifunga timu kubwa za Simba na Yanga ni baada ya kuifungia Polisi bao la kufutia machozi kwenye mchezo wao waliokubali kufungwa mabao 2-1 dhidi ya Simba.

Niyonzima, ambaye aliokosekana kwenye mchezo uliopita dhidi ya Tanzania Prisons kutokana na kusumbuliwa na malaria umuhimu wake ulionekana jana kutokana na kucheza vizuri eneo la kiungo, lakini timu haikupata matokeo.

Akicheza nafasi ya kiungo mshambuliaji akisaidiana na Mapinduzi Balama sambamba naTshishimbi, waliifanya Yanga kucheza kwa utulivu zaidi tofauti na mchezo uliopita ingawa kipindi cha pili kasi ya Polisi ilionekana kuwashinda. Baraka Majogoro, Matheo Antony na Marcel Kaheza waliichachafya Yanga mara kadhaa, lakini wakashindwa kuwafurahisha mashabiki wao ambao walisafiri kutoka maeneo ya Kishumundu, Marangu, Uru na Same kushangilia ushindi.

Bernard Morrison alionyesha makali yake, lakini hayakutosha kuipandisha Yanga kwenye msimamo.

Polisi ndio walianza kutengeneza nafasi katika dakika ya tatu ya mchezo, lakini umakini wa kipa wa Yanga, Farouk Shikalo ulisababisha washindwe kuwanyanyua mashabiki wao katika uwanja wa nyumbani. Yanga walikuwa wanatumia mfumo wa kupasiana pasi fupifupi hadi langoni kwa wapinzani kwao huku wapinzani wao wakitumia mfumo wa kupiga pasi ndefu ambazo zilikuwa zinazibutuliwa na mabeki wa Yanga.

Kipindi cha pili kilianza kwa timu zote kutegeana, lakini Polisi walionekana kuhitaji bao la kusawazisha kutokana na kuingia kwa kasi ya kuliandama zaidi lango la wapinzani wao.

Dakika ya 62, Polisi walifanya mabadiliko kwa kumtoa Majogoro na kumwingiza Mohamed Mkopi na Yanga walimtoa Tariq - mfungaji wa bao na nafasi yake kuchukuliwa na Yikpe Ghislain.

Yanga walifanya shambulizi la kushtukiza langoni mwa Polisi wakimtumia Morrison, ambaye alipiga shuti la mbali dakika ya 65 ambalo lilipanguliwa na kipa na kuzaa kona ambayo haikuwa na madhara langoni kwa Polisi. Katika dakika ya 67, Matheo Antony aliifungia timu yake bao la kusawazisha ambalo lilikataliwa na mwamuzi wa pembeni akithibitisha kuwa kabla ya kufunga alimfanyia madhambi Jaffar Mohamed.

Mabadiliko ya upande wa Yanga hayakuwa na madhara kwa polisi ambayo dakika ya 85 ilimtoa Niyonzima na kumwingiza Abdulazizi Makame, ambaye hata hivyo hakuwa na madhara.

Nahodha wa Polisi, Idd Mobby alisema walijiandaa kuibuka na ushindi, lakini imekuwa tofauti huku akimtolea uvivu mwamuzi kwa kukataa bao lao ambalo lingeweza kuwapa pointi tatu nyumbani.

NJE YA UWANJA

Kabla ya mchezo huo, Eymael alisema timu yake iligoma kuingia vyumbani kwa vile mazingira ni machafu na hayakuwa salama kwao.

Yanga walionekana wakiwa nje ya uwanja wakiwa na viti ili kuvitumia kukalia kwa wale ambao, wangekuwa benchi na maofisa wao.

Yanga: Farouk Shikalo, Juma Abdul, Jafari Mohamed, Kelvin Yondani, Lamine Moro, Papy Kabamba, Ditram Nchimbi, Haruna Niyonzima, Tariq Seif, Mapinduzi Balama na Benard Morrison.

Polisi: Mohamed Yusuf, Willium Lucian, Yassin Mustapha, Idd Mobby, Mohamed Kassim, Pato Ngonyani, Jimmy Shoji, Baraka Majogoro, Matheo Antony, Marcel Kaheza na Sixtus Sabilo.