Kikosi bora cha Ligi Kuu bara 2019/2020

Muktasari:

Wakati msimu ukifikia ukingoni, wapo wachezaji ambao wanapaswa kupata sifa stahiki kutokana na kiwango bora walichokionyesha ambacho kwa namna moja au nyingine kilikuwa na msaada kwa timu zao.

Katika kundi la zaidi ya wachezaji 500 waliozitumikia timu 20 zinazoshiriki Ligi Kuu, hapana shaka wapo ambao wamekuwa wakionyesha kiwango bora, lakini kuna wale wenye mchango wa wastani kwa timu zao na pia ambao wameonyesha viwango vya chini.

Wakati msimu ukifikia ukingoni, wapo wachezaji ambao wanapaswa kupata sifa stahiki kutokana na kiwango bora walichokionyesha ambacho kwa namna moja au nyingine kilikuwa na msaada kwa timu zao.

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) na Bodi ya Ligi Kuu (TPLB), wamekuwa na utaratibu wa kutoa zawadi kwa wachezaji waliofanya vizuri zaidi pindi msimu unapokuwa umemalizika, lakini pia huwa wanatangaza kikosi bora cha nyota 11 ambao wameonyesha viwango bora kulinganisha na wengine.

Hata hivyo, hilo huwa halizuii maoni na mijadala kutoka kwa wadau wa soka juu ya wachezaji waliofanya vizuri kwa msimu.

Mwanaspoti kama miongoni mwa wadau waliofuatilia kwa karibu Ligi Kuu msimu huu linakuletea orodha ya nyota 11 bora ambao walionekana kuwa na sifa za kipekee kulinganisha na wengine.

Hata hivyo, siyo lazima kikosi hicho kifanane au kiwe sawa na kile kitakachoteuliwa na mamlaka husika baada ya ligi kumalizika.

Wapo wachezaji wanaoweza kuwemo, lakini kuna ambao pengine watakosekana ingawa pia wote wanaweza wasiwemo katika kikosi cha msimu kitakachotangazwa na Kamati ya Tuzo ya TFF.

1. Aishi Manula – Simba  

Katika idadi kubwa ya ligi, kipa anayemaliza msimu akiwa hajaruhusu nyavu zake kutikiswa mara nyingi ndiye huteuliwa kuwa mlinda mlango bora wa msimu na pia jina lake huwemo katika kikosi cha msimu.

Kipa wa Simba, Aishi Manula licha ya kiwango bora ambacho amekionyesha msimu huu kwa kuondoa hatari na kuokoa michomo ya wapinzani, ndiye kipa ambaye anaongoza kwa kutoruhusu mabao katika idadi kubwa ya mechi (clean sheet) ambapo hadi sasa amecheza bila kuruhusu bao katika michezo 18 ya Ligi Kuu msimu huu.

2. Nico Wadada- Azam

Pamoja na majukumu ya ulinzi, beki bora wa pembeni ana kazi nyingine ndani ya uwanja ambayo ni kusaidia mashambulizi kwa timu yake.

Kwa upande wa beki wa kulia, mlinzi wa Azam FC, Nico Wadada ambaye ni raia wa Uganda ameonekana kutimiza vyema majukumu hayo mawili kulinganisha na wengine wanaocheza nafasi hiyo ambapo licha ya kufanya vyema katika kujilinda, amehusika katika jumla ya mabao tisa ya timu hiyo msimu huu akifunga moja na kupiga pasi nane zilizozaa mabao.

3. David Luhende - Kagera Sugar

Mlinzi wa Kagera Sugar, David Luhende ndiye mchezaji wa nafasi ya beki wa kushoto aliyefanya vizuri zaidi msimu huu kulinganisha na wengine wanaocheza katika nafasi hiyo.

Kwanza ndiye mchezaji ambaye amecheza mechi zote za Ligi Kuu msimu huu, lakini kana kwamba haitoshi ndiye beki wa kushoto aliyepiga pasi nyingi za mabao msimu huu ambazo ni tano.

4. Lamine Moro - Yanga

Kwa muda mrefu, safu ya ulinzi ya Yanga ilikuwa inamkosa beki wa kati kiongozi, lakini pengo hilo linaonekana kuzibwa vyema na Mghana Lamine Moro ambaye amekuwa muhimili imara wa safu ya ulinzi ya timu hiyo.

Licha ya kucheza na kundi kubwa la mabeki wenye kiwango cha wastani, Moro amekuwa msaada mkubwa kwa Yanga msimu huu na anapokosekana timu hiyo imekuwa ikifanya vibaya zaidi katika ulinzi.

5. Serge Wawa - Simba

Simba haikukosea kumpa mkataba mpya beki Serge Wawa ili aendelee kuitumikia timu hiyo msimu huu.

Uwezo wake wa kusoma na kudhibiti mbio za washambuliaji wa timu pinzani, kuwasiliana vyema na walinzi wenzake na kuchezesha timu kuanzia nyuma kumemfanya awe na namba ya kudumu katika kikosi cha Simba msimu huu.

6. Jonas Mkude - Simba

Simba ndio timu iliyoruhusu idadi ndogo ya mabao msimu huu, lakini hilo pengine lisingeweza kuwepo ikiwa wangekosa kiungo mwenye uwezo wa kutibua mipango ya wapinzani na kuziba njia zao.

Uwepo wa

Jonas Mkude umeiwezesha Simba kutoshambuliwa mara kwa mara na wapinzani na pia amekuwa na sifa nyingine ya kuichezesha timu pamoja na kufunga mabao ambapo ameifungia timu hiyo mabao mawili msimu huu.

7. Luis Miquissone - Simba

Alijiunga na Simba katika dirisha dogo la usajili, lakini ndani ya muda mfupi ameweza kugeuka tishio kwenye ligi na kutoa mchango mkubwa kwa timu yake.

Mabao manne aliyofunga na pasi tano za mabao alizopiga ni ishara tosha ya mchango wa Miquissone alioutoa kwa Simba ndani ya muda mfupi.

8. Clatous Chama - Simba

Jukumu kuu la kiungo mshambuliaji ni kuzalisha mabao iwe kwa kufunga ama kupiga pasi ya mwisho.

Mzambia Clatous Chama ameendelea kudhihirisha kuwa hana mpinzani katika hilo kwani ndiye kinara wa kupiga pasi za mwisho katika Ligi Kuu msimu huu.

Kiungo huyo kabla ya mechi ya mwisho ya ligi dhidi ya Polisi Tanzania alikuwa amepiga pasi 10 za mabao huku pia akiifungia Simba, mabao mawili.

9. Meddie Kagere - Simba

Kwa msimu wa pili mfululizo, Meddie Kagere ameendelea kuwa tishio katika kufumania nyavu, akiweza kurudia kile alichokifanya msimu uliopita ambacho ni kumaliza msimu akiwa mfungaji bora.

Mabao yake 22 yamemfanya awe mfungaji bora wa Ligi Kuu kwa mara ya pili mfululizo kama alivyofanya msimu uliopita alipopachika mabao 23.

10. Reliants Lusajo - Namungo FC

Ikishiriki kwa mara ya kwanza kwenye Ligi Kuu, Namungo FC imeweza kumaliza ikiwa katika nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi.

Hata hivyo nahodha wao Reliants Lusajo anapaswa kupata pongezi za kipekee kwa kuongoza kwa mfano na vitendo, akiifungia timu hiyo mabao 12 katika Ligi Kuu msimu huu

11. Yusuph Mhilu - Kagera Sugar

Licha ya kuchezeshwa nafasi ya winga, Mhilu amekuwa mwiba kwa nyavu za timu pinzani kutokana na uwezo mkubwa wa kufumania nyavu alioonyesha. Mabao yake 13 aliyofunga katika Ligi msimu huu yamekuwa ni kama sukari iliyopamba keki ya kiwango bora alichoonyesha katika mechi za Kagera Sugar.

Kocha - Hitimana Thiery

Uwepo wake katika kikosi cha Namungo FC umechangia kwa kiasi kikubwa timu hiyo kumaliza ikiwa katika nafasi nne za juu kwenye msimamo wa Ligi Kuu.

Ameweza kutengeneza muunganiko bora wa kitimu katika kikosi cha Namungo lakini ameweza kuimarisha kiwango cha mchezaji mmojammoja.

Pamoja na hilo ameweza kujenga hali ya kujiamini kwa timu yake na pia kimbinu hali inayoifanya icheze soka la kuvutia na la ushindani.

Akiba

Daniel Mgore- Biashara United

Feisal Salum- Yanga

Shomary Kapombe- Simba

Stephen Duah- Namungo

Lucas Kikoti- Namungo

Deo Kanda- Simba

Martin Kiggi- Alliance