Kikosi ‘kipana’ Simba SC chazua mijadala

Dar es Salaam. Wakati kauli ya Simba ya kikosi kipana ikionekana kuacha maswali, nyota wa zamani wa timu hiyo wametoa tathmini yao kuhusu upana wa kikosi hicho kuelekea kwenye mashindano ya kimataifa huku wakimshauri kocha Sven Ludwig van den Broeck.

Simba ilicheza ugenini bila nyota wake sita, Clatous Chama, Meddie Kagere, Chris Mugalu, Serge Wawa, Gérson Fraga na John Bocco na kuruhusu kipigo cha bao 1-0.

Bocco na Kagere waliachwa Dar es Salaam kutokana na majeruha, Mugalu aliumia dakika za mwisho kabla ya mechi, Chama na Wawa wameenda kwao, Fraga pia ni mgonjwa.

Kukosekana kwa nyota hao na kipigo cha juzi vimeibua maswali huku baadhi ya wadau wakihoji ni vipi kikosi kipana kimeonekana kupwaya baada ya wachezaji hao kukosekana.

“Maana ya kikosi kipana ni kuwa na timu mbili zenye uwezo sawa kwa wakati mmoja na kukupa matokeo, ila kwa mazingira ya mechi ya jana (juzi), Simba inapwaya,” alisema kipa wa zamani, Mosses Mkandawile.

Malota Soma alisema wachezaji sita kukosekana kwenye timu ni wengi na kama ni tegemeo basi lazima timu itapwaya na ndicho kimewakuta Simba juzi.

“Simba ina kikosi kipana sawa, lakini wachezaji wengine hawapati nafasi ya kuonekana, ikitokea wamepata nafasi wanashindwa kuendana na kasi, kocha angeweka mfumo hata kama mchezaji fulani hayupo, kuna mtu mbadala,” alisema Mkandawile.

Mbali na nyota hao, kocha Abdul Mingange wa Lipuli alitaja mambo mawili yanayoisumbua Simba ambayo ni aina ya uchezaji, lakini pia anafikiri kocha Sven ni kama hawaamini baadhi ya wachezaji wake, kitu ambacho kimewagharimu juzi walipopata nafasi.