Kikapu wakunwa michuano BBall Kings

Muktasari:

Akizungumza Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Ufundi wa TBF, Manase Zabroni alisema ushindani wa mashindano hayo mwaka huu ni mkubwa kwa kuwa timu zote zimefanya maandalizi ya kutosha.

Dar es Salaam. Wakati mashindano ya mpira wa kikapu Sprite BBall Kings yakiingia hatua ya robo fainali, Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF), limevutiwa na mchuano mkali wa timu zinazoshiriki michuano hiyo.

Akizungumza Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Ufundi wa TBF, Manase Zabroni alisema ushindani wa mashindano hayo mwaka huu ni mkubwa kwa kuwa timu zote zimefanya maandalizi ya kutosha.

Zabroni, alisema hakuna timu ya kubeza katika mashindano hayo kwa kuwa kila moja imeingia katika king’anyiro hicho ikiwa na malengo ya kutwaa ubingwa.

“Msimu huu timu zimejiandaa vizuri ndio maana tumeshuhudia mechi nyingi zikiwa na ushindani mkali, tuna amini mwaka huu bingwa atapatikana kwa taabu,” alisema Zabroni.

Mashindano hayo yameingia katika hatua ya robo fainali na mwishoni mwa wiki timu nne ziliteremka kwenye viwanja viwili tofauti Airwing na Bandari, Dar es Salaam kuwania ushindi.

Timu ya DMI ilishinda mabao 113-64 ilipovaana na Fast Heat kabla ya Flying Dribbellrs kuinyuka Hitmen 87- 63.

Pia St Joseph iliibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 98- 78 dhidi ya Airwing kabla ya Portland kuinyuka Mbezi Beach 126-54.

Nayo Mchenga BBall Stars iliilaza Oysterbay mabao 117-56, Temeke Heroes iliinyuka Stylers 76-58. Team Kiza ilishinda 66-56 ilipovaana na Ukonga Warriors, Water Institute iliinyuka Raptors 77-68.

Mechi nyingine ya mashindano hayo iliwapeleka Team Kiza robo fainali kwa ushindi wa mabao 66-56 dhidi ya Ukonga Warriors.