Kikapu, riadha kushiriki mashindano ya Afrika

Muktasari:

  • Michezo hiyo inafanyika Rwanda kwa ajili ya kumbukumbu ya mauaji ya Kimbari yaliyotokea nchini humo mwaka 1994, nchi nyingine zitakazoshiriki ni wenyeji Rwanda, Kenya, Uganda, Sudan Kusini, Ethiopia, Eritrea, Sudan, Somalia na Misri.

Dar es Salaam. Timu za mpira wa kikapu na riadha zimetajwa kuiwakilisha nchi kwenye Michezo ya Vijana ya Kanda ya Tano ya Afrika itakayofanyika Kigali, Rwanda.

Katika michezo hiyo itakayoanza Aprili 2hadi 6 ambayo ni maalum kwa kumbukumbu ya Mauaji ya Kimbari, Tanzania itawakilishwa na wanamichezo tisa na makocha wawili.

Timu hiyo ya wachezaji chini ya miaka 18 itaondoka nchini Machi 31.

Katibu Mkuu wa Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC), Filbert Bayi amesema timu ya riadha itakuwa chini ya kocha Mwinga Mwanjala.

Wanariadha ni Regina Mpigachai (atakayekimbia mbio za mita800 na 1500), Amosi Charles (mita 400), Gaundencia Maneno (1500), Ester Martin (mita 3,000) na Francis Damas (mita 5,000).

Alisema kuwa kocha wa timu ya mpira wa kikapu ni Phineas Kahabi.

Wachezaji ni Josephat Sanka, Charles Majombo, Daud Maiga na Ally Abdallah.

Alisema timu ya mpira wa kikapu itashiriki mchezo wa wachezaji watatu watatu, huku ikiwa na mchezaji mmoja wa akiba.