Ligi Kuu Wanawake yaacha vumbi Kigoma

Monday December 11 2017

 

By Charles Abel

TIMU ya Kigoma Sisters jana Jumapili imemaliza kwa kishindo hatua ya makundi ya Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania kwa kuichapa Alliance Girls kwa bao 1-0 katika mechi iliyochezwa uwanja wa General Tyre jijini Arusha.

Ushindi huo umeifanya Kigoma Sisters kumaliza kileleni mwa msimamo wa kundi B ikiwa na pointi 15 baada ya kuibuka na ushindi katika mechi zote tano ilizocheza dhidi ya Majengo Queens, Baobab, Panama, Marsh Girls na Alliance Girls.

Bao lililowapa ushindi Kigoma Sisters lilifungwa dakika ya  65 na  Mukamana Clementine kupitia mpira wa  kona iliyokwenda moja kwa moja nyavuni.

 

Afisa Habari wa Alliance Girls, Jackson Mwafulango alisema timu yake imeridhishwa na matokeo licha ya matarajio waliyokuwa nayo.

 

"Malengo yetu yalikuwa ni kutopoteza mechi lakini kwa bahati mbaya tumepoteza licha ya kiwango kikubwa tulichoonyesha.

 

Tumemaliza tukiwa nafasi ya pili na pointi 10 na kwa sasa tunakwenda kujipanga kwa ajili ya hatua ya nane bora," alisema Mwafulango