Kigogo Yanga ajilipua Msimbazi

Muktasari:

  • Bosi wa zamani wa Yanga, Abdul Sauko ameibuka na kuwapiga 'dongo' Watani wao wa Jadi Simba kuwa wako vizuri kiuchumi kuliko timu yake, lakini uwanjani ni wepesi tu na kama si pesa za tajiri yao, Mohammed Dewji 'Mo' wangelia.

NI kweli kwa sasa Simba wapo vyema kiuchumi kuliko Yanga, lakini bosi wa zamani wa klabu hiyo Abdul Sauko ameibuka na kudai kuwa watani zao ni wepesi tu na ndio maana wamekuwa na matokeo ya kuungaunga zaidi kuliko Jangwani ambao wameyumba kiuchumi.

Katibu Mipango huyo wa zamani enzi za uongozi wa Tarimba Abbas, alisema Simba wanapaswa kumshukuru mwekezaji wao, Mohammed ‘MO’ Dewji kuwastiri vinginevyo wangekuwa pabaya kuliko Yanga wanayoibeza kwa kutembeza bakuli kwa mashabiki.

Sauko alisema ni kweli Simba wapo vizuri kiuchumi kutokana na uwekezaji MO Dewji, lakini bado hawapo vizuri uwanjani kama matarajio ya wengi, huku Yanga ikiwa ovyo kiuchumi lakini wakionekana bora kwa matokeo iliyopata katika mechi zake za Ligi Kuu.

“Simba wanapaswa kutofautisha suala la kuwa na uwezo kiuchumi na soka uwanjani, wana fedha ambazo sisi hatuna, ila hawana soka tulilonalo sisi na ukitaka kujua ukweli angalia pambano la watani wiki iliyopita,” alisema Sauko.

Alisema licha ya Yanga kupitia hali ngumu kiuchumi, alidai wameanza kwa kishindo kuliko watani wao Simba na jambo kubwa alilolisisitiza kwa Wanajangwani ni kushikamana na kuwa wazalendo ili kuendelea kushangaza wadau wa soka nchini.

“Tuendelee kudumisha mshikamano wa kweli, tujenge uzalendo kwa timu ambao hata kama hatupo vizuri kiuchumi, ila wachezaji wawe mwiba dhidi ya timu wanazoshindana nazo kwenye ligi, hilo linawezekana ni maamuzi tu ya kila shabiki wa Yanga.

“Ni kweli Yanga inahitaji pesa itakayofanya wachezaji waandaliwe vyema na kuwatimizia mahitaji yao kwa wakati, lakini pia kile wanachokifanya wachezaji uwanjani, kinapaswa kuungwa mkono kwa asilimia 100, tukifanya hivyo itakuwa ni dawa tosha ya kuwavuruga wapinzani,”alisema.

Akiizungumzia ligi kwa ujumla alisema imeanza kwa kasi ya ajabu, inayotoa taswira ya timu zimebadilika na zinahitaji kuonyesha kitu cha kipekee, tofauti na miaka ya nyuma.