Kigogo El Jadida ambania Msuva safari ya Ulaya

Monday January 14 2019

 

By Eliya Solomon

BOSI wa Difaa El Jadida, Abdelatif Moktarid ameingilia kati inshu ya mshambuliaji wa Kitanzania, Saimon Msuva kuondoka kwenye klabu hiyo kipindi hiki cha dirisha dogo la usajili Morocco.

Kuna taarifa Msuva ambaye alikuwa akiichezea Yanga ya jijini Dar es Salaam kabla ya kujiunga na Difaa El Jadida, amekuwa kwenye rada za Kasımpa inayoshiriki Ligi Kuu Uturuki kwa kipindi kirefu.

Hii ni mara ya pili kwa Msuva kuzuiwa. Mara ya kwanza ilikuwa mwanzoni mwa msimu huu wa 2018/19 ambapo inadaiwa Difaa iliwekewa ofa kadhaa mezani lakini ilizigeuzia kisogo.

Akizungumza na Nje ya Bongo, nyota hiyo anayeitumikia pia Timu ya Taifa ya Tanzania alisema mara zote Moktarid amekuwa akimweleza kinachoendelea na kikubwa amekuwa akimtaka kuwa mvumilivu kwa kutokuwa na papara ya kuondoka.

“Ninahitaji kwenda kucheza soka Ulaya na makubaliano yangu na Moktarid yalikuwa ni kuondoka kipindi hiki kwa hiyo nimesikitika sana kwa kuamua kusogeza mbele uhamisho wangu.

“Mwanzoni mwa msimu waliniwekea ngumu kuondoka kutokana na idadi kubwa ya wachezaji waliowauza, nilimwelewa na nilibaki kama mchezaji pekee ambaye waliyekuwa wakinitegemea kwenye safu ya ushambuliaji.

“Sipendi kuwa mlalamishi ila natakiwa kuvumilia hadi mwishoni mwa msimu maana bado nina mkataba na Difaa, nataka niondoke hapa kwa amani, kikubwa ni kuendelea kukaza ili niendelee kuzivutua klabu nyingine kubwa,” alisema Msuva.

Huu ni msimu wa pili kwa Msuva kuichezea Difaa, katika msimu wake wa kwanza kwenye Ligi ya Morocco, Batola Pro aliipachikia timu hiyo mabao 11 ambayo yalimfanya kuwa kinara wa mabao kwenye klabu yake.

Msimu huu ambao ulianza vibaya kwa Msuva kubadilishwa namba amepachika mabao manne kwenye michezo minne ya Batola Pro huku kinara wa mabao wa ligi hiyo akiwa Mtogo, Kodjo Laba mwenye mabao 10 wa RSB Berkane.

“Bado nitapambana tu, najua kiu yangu na Watanzania wenzangu ni kuniona nikisonga mbele, lakini mambo bado hayajakuwa mazuri, naendelea kumuomba Mungu, iko siku nitapiga hatua,” alisema.

Advertisement