Kifo cha msanii Tanzania chazua utata, ndugu wataka uchunguzi

Muktasari:

Kufuatia utata uliogubika kifo cha msanii wa muziki nchini Tanzania, Mbalamwezi kutoka kundi la The Mafik, ikiwamo gitaa na mwili wake kukutwa maeneo tofauti huku mwili ukia umevuliwa nguo, familia yataka uchunguzi ufanyike kubaini kama kuna mkono wa mtu.

Dar es Salaam. Chief Mponda, ambaye ni mjomba wa marehemu msanii wa muziki nchini Tanzania, Abdallah Matimbwa maarufu ‘Mbalamwezi’ kutoka kundi la The Mafik amesema kifo cha mtoto wao huyo bado kinawapa maswali mengi.

Mponda akizungumza na Mwananchi leo Ijumaa Agosti 16, 2019 amesema Mbalamwezi amekutwa amekufa kituo kilichofuata maeneo ya Mbezi huko gitaa lake likiwa Mbezi Jogoo, Dar es Salaam.

Mjomba huyo anayesema bado mpaka sasa hivi hawajauona mwili wa mtoto wao huyo lakini wamepata maelezo kutoka kwa Polisi maeneo waliyomkuta amekufa.

Mbali na gitaa kuwa eneo tofauti, amesema na nguo alikuwa kavuliwa , “mtu gani anagongwa na gari na nguo zote kuvulika?. 

Vilevile amesema wameambiwa ameumia maeneo ya mapajani na kueleza kuwa kwa mazingira hayo ni wazi kwamba kuna mkono wa mtu na kutaka uchunguzi ufanyike.

Kuhusu mazishi, amesema wanatarajia kuyafanya kesho Jumamosi Agosti 17,2019 na msiba upo Tandika mtaa wa Mindu.