Kidao amwaga ushahidi Kisutu

Muktasari:

  • Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha kuwa miongoni mwa mashtaka  ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana huku wenzao Zayumba na Frola wapo nje kwa dhamana.

KESI inayowakabili viongozi wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) imeanza kunoga baada ya Katibu Mkuu wa sasa wa Shirikidho hilo, Wilfred Kidao kutoa ushahidi akiieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa, tangu awe Mjumbe wa Kamati ya Utendaji mwaka 2013- 2017 hajawahi kuona maombi kuhusu TFF kukopeshwa fedha na mtu binafsi.

Kidao aliyaeleza hayo jana Jumatano mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri wakati akitoa ushahidi katika kesi inayomkabili aliyekuwa Rais wa TFF, Jamal Malinzi na wenzake wanne.

Shahidi huyo wa nane wa upande wa mashtaka alitoa maelezo hayo baada ya kuulizwa awali na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Leonard Swai amewahi kuona maombi ya mshtakiwa wa kwanza ya kuikopesha Fedha TFF.

“Sijawahi kuona maombi ya TFF kukopeshwa fedha, wala hatujawahi kuona maombi kuhusu mtu binafsi kuikopesha Fedha TFF,” alisema Kidao.

Alidai utaratibu wa TFF ambayo ni Taasisi inapohitaji kukopa Fedha huwa inaomba ridhaa ya Kamati ya Utendaji na kwamba hiyo ni kwa mujibu wa kanuni za Fedha za TFF.

Aliongeza maombi hayo huwasilishwa kwa njia mbili ya kwanza vikao na pili kuwatumia wajumbe waraka kwa barua pepe na hujibu kwa kukubali ama kukataa na Kidao alidai kama Katibu Mkuu hajawahi kupata madai yoyote ya mrejesho.

Shahidi huyo aliendelea kutoa maelezo kuwa mambo yote yanayohusu fedha yanapaswa kupitishwa na Kamati ya Utendaji na kuhidhinishwa na Mkutano Mkuu wa TFF.

Baada ya shahidi huyo kwa upande wa mashtaka kueleza hayo, kiongozi wa jopo la mawakili wa utetezi, Richard Rweyongeza alimuuliza unakumbuka kuna kipindi akaunti ya TFF ilifungiwa.

Kidao alijibu kuwa mara nyingi akaunti ya TFF imekuwa ikipata matatizo ya kufungiwa.

Wakili Rweyongeza alimuuliza Kidao, kama Katibu Mkuu na Utendaji Mkuu wa TFF, nani katika shirikisho hilo analalamika kwamba Fedha za TFF zimeibwa na washtakiwa, Malinzi, Msigwa na Nsiande Mwanga.

Kidao akijibu “ Mimi bado hatujapata taarifa za ukaguzi wa mahesabu ya fedha ya mwaka uliopita hadi sasa, ripoti tunaifanyia kazi, bado haijatoka, tunasubiri hivyo hatujawahi kusema mtu ametuibia” alieleza Kidao.

Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa leo. Washtakiwa katika kesi hiyo mbali na Malinzi, wengine ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Selestine, Mhasibu wa TFF, Nsiande Mwanga, Meneja wa Ofisi ya TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 30 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.