Kichuya awapagawisha Asante Kotoko

Thursday August 9 2018

 

By DORIS MALIYAGA

 Dar es Salaam. Kocha Mkuu wa Asante Kotoko, Samwel Kwasi amemvulia kofia kiungo wa Simba, Shiza Kichuya.
Akizungumza baada ya mchezo huo uliomalizika kwa sare ya 1-1, kocha Kwasi  alisema mchezaji aliyevutia ndani ya kikosi cha Simba ni yule mfupi ambaye amevaa jezi namba 25 (Kichuya).
“Ameonyesha kiwango cha juu na alicheza kwa kasi kwangu ndiye aliyekuwa na madhara katika mchezo huu."
Kauli hiyo inafanana na wachezaji wake, Nafiu Awudu Mghana aliyewahi kuichezea Azam FC miaka ya nyuma na Obed Awusu, lakini wao waliongeza na Jonas Mkude pamoja na Chama.
Awudu amesema: "Kwangu wachezaji watatu, namba 20 (Mkude), 25 (Kichuya) na 27 (Chama) ndiyo walikuwa injini ya Simba katika mchezo huu. Walichezesha timu kwa ufasaha."
Awusu amesema, Simba imecheza mchezo mzuri, lakini aliyemvutia ni Kichuya: "Yule mfupi namba 27, anajua sana."
Katika hatua nyingine mashabiki wa Simba walimpa kitambaa cha klabu hiyo beki wa Asante Kotoko, Agyeman Badu wakionyesha kuvutiwa na soka lake.
"Wamenipa mashabiki wa Simba, kwangu ni furaha na ukumbusho mkubwa," alisema Badu na kueleza kama Wekundu hao watakuwa tayari kumsajili atakuwa tayari.