Kichuya ampa Himid Mao mbinu za kutoboa ENNPIA

Wednesday August 14 2019

 

By Olipa Assa

Dar es Salaam.Winga wa zamani wa Simba, Shiza Kichuya amesema kwa aina ya uchezaji wa Himid Mao aliyesaini kwenye klabu ya ENNPI ya Misri aliyoichezea yeye kwa mkopo, anaamini atafanya vitu vya kustajabisha ambavyo vitamfanya afike mbali.

Kichuya alifunguka kamba licha ya kukaa muda mfupi ndani ya klabu hiyo, alidai alifanikiwa kujifunza mambo kwa sehemu anayoamini ataendelea kuyafanyia kazi, akiamini yatampa matunda.

Alizungumzia nafasi ya Himid ndani ya kikosi hicho kwamba anaiona ana nafasi kubwa ya kuanza moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza, akimshauri apate muda wa kuyasoma mazingira kwa haraka haraka.

"Himid akipata muda wa kusoma mazingira akayazoea kwa haraka, atakuwa na mafanikio ndani ya kikosi hicho kwani anatumia nguvu na akili, hivyo namwamini kwamba atafanya vitu vikubwa,"alisema Kichuya.

Himid alisema anatambua nini kimempeleka kucheza soka la nje, hivyo anaamini ataiwakilisha vyema bendera ya Tanzania na kufanyika kuwa njia kwa watu wengine kupata nafasi ya kucheza Misri.

"Nje ni nje tu, soka la huku lipo juu lakini nitapambana kadri niwezavyo kuhakikisha nafanya vizuri ambako kutafanya niwe msaada kwenye timu ya Taifa Stars na ndivyo ilivyo kwa mataifa mengine wanacheza soka la kulipwa wakirejea kwenye mataifa yao wanakuwa hatari,"alisema.

Advertisement

Advertisement