Kichuya afunguka kukosa mabao Simba

Muktasari:

Mshambuliaji wa Simba Shiza Kichuya amesema kuwa bao alilofunga dhidi ya African Lyon, limempa morari ya kufunga mabao mengi katika Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Kichuya alisema tangu msimu huu, ameshindwa kufunga idadi kubwa ya mabao kwa kuwa kocha amempangia majukumu mengine ndani ya uwanja.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Simba, Shiza Kichuya amesema ametoa sababu ya kutofunga mabao katika mashindano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu.

Akizungumza Dar es Salaam, Kichuya alisema upangaji wa kikosi ni miongoni mwa mambo yaliyochangia kushindwa kufunga mabao katika Ligi Kuu.

"Kufunga inategemea na nafasi unayopata lakini wengi hawajui kuwa wakati mwingine kocha ananipa majukumu tofauti, hivyo  nakuwa sina nafasi kubwa ya kufunga kama wengi wanavyotaka,” alisema Kichuya.

Mchezaji huyo alitoa kauli hiyo baada ya kufunga bao la kwanza msimu huu dhidi ya African Lyon, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kiungo huyo wa pembeni, ameanza vibaya msimu na kiwango chake kimeonekana kuporomoka licha ya kupata namba katika kikosi cha kwanza.

Kichuya alisema amekuwa akitafuta nafasi ya kufunga kujenga hali ya kujiamini na bao dhidi ya African Lyon limemuongezea morali ya kufanya vyema katika Ligi Kuu.

Mchezaji huyo ameachwa katika kikosi cha Taifa Stars ambacho kiliondoka juzi usiku kwenda Cape Verde kucheza mchezo wa kufuzu fainali za Afrika. Timu hizo zitacheza Ijumaa usiku.

Kocha Mohammed ‘Adolf’ Rishard alisema Kichuya anatakiwa kubadili mbinu ya uchezaji baada ya kupangiwa majukumu mengine na kocha.

“Sikubaliani na watu wanaosema Kichuya ameshuka kiwango, nafuatilia mechi nyingi za Simba ambazo amecheza nimeona kila akitolewa Simba inayumba,” alisema kocha Mrage Kabange.