Kichuya: Yanga inakula nyingi tu

Muktasari:

  • Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka nchini Misri, Kichuya alisema Simba inahitaji utulivu, umakini na kuangalia upenyo wa kufunga mabao dhidi ya Yanga akiamini watatoka kifua mbele Uwanja wa Taifa, keshokutwa Jumamosi.

NYOTA wa kimataifa wa Tanzania, Shiza Kichuya anayecheza soka la kulipwa Misri katika klabu ya ENPPI kwa mkopo akitokea Pharco FC ya Daraja la Pili, amesema anaipa nafasi kubwa Simba kuifumua Yanga katika Kariakoo Derby, kutokana na kuwa na safu kali na yenye uchu wa mabao.

Hata hivyo Kichuya aliyeichezea Simba kabla ya kwenda ENPPI, alisema Wekundu wanaweza kushinda dhidi ya Yanga endapo tu wataongeza umakini wa mahesabu yao ndani ya dakika 90.

Kichuya aliyekuwepo kwenye mchezo wa kwanza uliopigwa Septemba 30, mwaka jana na kumalizika kwa suluhu, alisema Simba ina nafasi kubwa ya kushinda kwenye Uwanja wa Taifa, hasa baada ya kutoka kushinda dhidi ya Al Ahly katika Ligi ya Mabingwa Afrika.

Katika mechi za watani wa jadi, Kichuya ameacha rekodi ya kuifunga Yanga mara tatu mfululizo.

Akizungumza na Mwanaspoti kwa njia ya simu kutoka nchini Misri, Kichuya alisema Simba inahitaji utulivu, umakini na kuangalia upenyo wa kufunga mabao dhidi ya Yanga akiamini watatoka kifua mbele Uwanja wa Taifa, keshokutwa Jumamosi.

“Kwanza hawapaswi kuwabeza Yanga ambao wanaongoza ligi, waingie wakiwa na nia ya kupambana kuhitaji pointi tatu na sio jambo lingine, wakidhamiria wataweza”

“Ukiangalia kikosi cha Simba kina wachezaji wazoefu safu ya ushambuliaji kuna Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco, Yanga wanamtegemea Heritier Makambo na Ibrahim Ajib, ambaye kiasili sio straika”alisema.

Alisema mechi ya watani ina presha kubwa kutoka kwa mashabiki, ila neno lake kubwa kwa Simba ni kuwa anaamini Okwi, Kagere na Bocco hawatamwangusha.

“Wasiingie kwa presha watulize mzuka naamini Simba itashinda na pia waangalie wachezaji ambao wapo vizuri upande wa pili wawe makini kuwalinda,”alisema.