Kichuya: Kama Al Ahly walipigwa, AS Vita nani?

Muktasari:

Kichuya amesema kama Simba iliweza kuifunga Al Ahly Uwanja wa Taifa, hakuna kitakachowazuia kuibuka na ushindi dhidi ya As Vita ya Kongo.

WINGA wa zamani wa Simba, Shiza Kichuya anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya ENPPI ya nchini Misri amewataka mastaa wa Msimbazi kuandika historia kwenye mechi yao na As Vita, inayopigwa saa 1:00 jioni.
Kichuya amesema kama waliweza kuwafunga Al Ahly Uwanja wa Taifa hakuna maajabu kuibuka na ushindi dhidi ya As Vita ya Kongo.
"Wapo wachezaji ndani ya Simba ambao wana uzoefu mkubwa na michuano ya kimataifa, watulize akili, nidhamu ya mchezo ihusike kwa asilimia 100 na kuondoa presha ya kufungwa mabao 5-0 ugenini, wanapaswa wajiamini na kujivunia kuwa nyumbani.
"Mechi ni ngumu lazima wapambane  wakishinda watakuwa wameingia kwenye historia nyingine ya kuleta heshima kwa nchini ya Tanzania, hivyo Watanzania hawana budi kuwaunga mkono ili wapate nguvu ya kujituma.
"Wanachokifanya Al Ahly na Kongo wanaibeba nchi mabegani mwao ndivyo hata mastaa wa Simba wanatakiwa kufanya hivyo ili waweze kuingia kwenye rekodi mpya.
"Safu ya ushambuliaji ya Simba, nina imani  na Meddie Kagere, Emmanuel Okwi na John Bocco kwamba watafanya kitu kikubwa kwenye mechi ya leo, nawaombea kila raheli ya kuibeba nchi na kuwapa furaha mamia ya watu ambao watafika uwanjani kuwaunga mkono,"anasema.