Kibwana: Huku Chama kule Morrison patamu

Tuesday June 23 2020
kibwana pic

LICHA ya kucheza kama beki wa kulia na anavaana washambuliaji wa pembeni wasumbufu, lakini anachoshukuru ni kwamba tangu aanze kucheza soka la ushindani hajawahi kuonyeshwa kadi nyekundu kutokana na uumini wake katika suala zima la nidhamu.

Kibwana Shomary ni mtu ambaye huenda mashabiki wa Yanga wakawa hawana hamu naye kutokana na kuwalaza njaa kwenye michuano ya Kombe la Mapinduzi 2020 kwa kusawazisha bao jioni katika mechi ya nusu fainali na kisha kwenda kuwazamisha kwa mikwaju ya penalti.

Kibwana aliyeibukia kwenye kikosi cha timu ya taifa U17, Serengeti Boys amefanya mahojiano na Mwanaspoti na kuweka bayana mambo mbalimbali ikiwamo safari yake kisoka na jinsi alivyopata sapoti kubwa kutoka kwa familia yake iliyomuunga mkono hadi kufika alipo.

Pia ameeleza changamoto anazokutana nazo na namna alivyo na ndoto za kufika mbali, huku akiwataja wachezaji saba katika skwadi lake la nguvu la Ligi Kuu Bara msimu huu akimtupa Clatous Chama huku, kule akimweka Bernard Morrison. Unajua wengine aliowataja? Endelea naye...!

AMPA TANO MBAPPE

Kibwana amecheza kikosi kimoja na nyota mbalimbali ndani ya Serengeti Boys na Ngorongoro Heroes na anasema straika Kelvin John ‘Mbappe’ ni moto mkali na sio mtu wa mchezo.

Advertisement

Beki huyo anasema Mbappe ni mchezaji wenye kipaji na anamuona akifika mbali hasa kutokana na juhudi zake, anataja kuwa Mbappe ni mchezaji aliyefanikiwa kucheza nje akiwa na umri mdogo na hicho ni kitu kinachomtia nguvu kupambana naye afike alikofikia straika huyo kinda.

“Ni mchezaji mzuri na namuona mbali zaidi ya alipo sasa. Ana kipaji na bahati pia. Kila mchezaji aliyekuwa naye Serengeti analijua na hata taifa linafahamu ukweli huu juu ya Mbappe.”

MECHI YAKE BORA

Kibwana anasema mechi dhidi Congo Brazzaville U17 iliyopigwa Taifa Septemba 18, 2016 ndio mechi bora kwake sio kwa sababu ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-2, bali ushindani mkubwa ulionyeshwa na timu zote siku hiyo.

“Ilikuwa mechi ya kufuzu Afcon U17, kwangu ndio bora kwani ilikuwa na ushindani mkubwa sana na pia niliupiga mwingi sambamba na wenzangu na kuibuka washindi,” anasema Kibwana.

AJIPENYEZA MSIMBAZI

Kibwana anakiri anakikubali sana kikosi cha Simba kwa kubaini ndio timu yenye kikosi kipana kwa sasa nchini na timu inayoundwa na wachezaji wenye uwezo mkubwa na vipaji, lakini bado anadhani kama angesajiliwa Msimbazi, asingekosa namba ya kukinukisha katika kikosi cha kwanza.

“Sio siri Simba wana kikosi kipana, hakuna mchezaji ambaye alisajiliwa pale kwa kuaminishwa kuwa yeye ni namba moja kikosini jitihada ndio zinatoa nafasi ya kucheza, hivyo kwa kukiangalia kikosi kile bado naiona nafasi kama ningesajiliwa kule,” anasema Kibwana.

CASSIAN PONELA AMBANIA

Kibwana anasema tangu anacheza soka utotoni alikuwa akipenda kuvaa jezi namba 12, lakini wakati anatua Mtibwa Sugar alikuta jezi hiyo ikivaliwa na Cassian Ponela.

Anasema kuikosa namba hiyo alipopandishwa katika kikosi cha wakubwa, ilimfanya achague jezi namba 29 anayoitumia hadi sasa, lakini roho inamuuma kwangu 12 ni namba anayoipenda kinoma kwani hata timu ya Serengeti na Ngorongoro amekuwa akiivaa.

“Napenda kuvaa jezi namba namba 12 ni jezi ambayo nilikua naitumia tangu udogoni, naipenda tu imenikuza, kwa sasa navaa namba 29 ambayo ndio niliyopewa baada ya kupandishwa nikitokea kikosi cha vijana, bro Cassian ndio anaitumia Namba 12 buana,” anasema Kibwana.

HUKU CHAMA KULE MORRISON

Beki huyo ameiangalia Ligi Kuu Bara msimu huu na kubaini imekuwa na ushindani mkubwa na wachezaji wanajituma kinoma na alipotakiwa kutaja kikosi chake bora, amewajumuisha nyota saba wa Simba na mmoja wa Yanga, sambamba na wengine wa Mtibwa.

Kibwana anasema kwa mtazamo wake na aina ya wachezaji walivyokiwasha hadi sasa ndani ya msimu huu, skwadi lake linaundwa na kipa, Aishi Manula, huku kulia akimtupa Shomary Kapombe, kushoto Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na beki ya kati ikiwa na Dickson Job na Erasto Nyoni.

“Viungo ni Jonas Mkude, Bernard Morrison na Clatous Chama, huku washambuliaji wakiwa ni John Bocco na Salum Kihimbwa na kocha wa kikosi hicho ni Mzazi, Zuberi Katwila,” anasema kwa skwadi hilo Chama akisimama huku na Morrison kule na Kihimbwa na Bocco mbele, lazima mtu apigwe nyingi tu kwani kule nyuma kutakuwa na ukuta wa chuma chini ya Nyoni.

U17 GABON HAINA MFANO

Kibwana alikuwa kwenye kikosi kilichoshiriki Fainali za Afcon U17 kule Gabon na anakiri zile zilikuwa fainali bab- kubwa kwake, lakini hataisahau mechi yao ya mwisho ya kundi ya kuwania kufuzu fainali za Kombe la Dunia na kutinga nusu fainali ya michuano hiyo.

“Serengeti ilikuwa inahitaji ushindi au kupata sare ili ifuzu, lakini ikajikuta ikalazimishwa sare ya 1-1, lakini tulifungwa bao 1-0 na kuifanya mechi hii ibaki akilini mwangu kwani ilitunyima nafasi ya kuandika historia,” anasema.

KIPAGWILE NOMA SANA

Kuhusu mchezaji anayemsumbua uwanjani, Kibwana hafichi. Anamtaja Idd Kipagwile wa Azam FC kwamba akikutana naye nyasi huwa hazina amani kabisa, unaweza kuhisi kuna Vita ya Tatu ya Dunia.

Anasema hayo yote yanatokea kwa vile ni mchezaji mzuri ana nguvu anacheza kwa akili.

“Kumkaba Kipagwile ni lazima ujipange ni mchezaji msumbufu kukabana naye, wengine nawaona wa kawaida sana,” anasema.

ELFU 15 YAMUINGIZA UWANJANI

Wakati anaanza maisha ya soka, Kibwana amewahi kucheza ndondo na posho yake ya mechi hiyo ilikuwa ni elfu 15 ambayo anasema ilimsaidia kununua baadhi ya vifaa vya mazoezi.

“Nilicheza ndondo ilikua ligi ya jezi nikapata Sh.15,000 ambayo ndio niliitumia kununua vifaa vya mazoezi. Timu ni ‘Black Viba’,” anafafanua Kibwana.

Kuhusu mabeki wa kulia, nafasi anayocheza Kibwana anasema Juma Abdul na Shomary Kapombe ndio anaowakubali, hata hivyo hakutaka hakutoa sababu za kuwakubali.

“Kwa ndani nawakubali na kuvutiwa na Kapombe, Abdul na Salum Kanoni, ila kwa nje ni Dani Alves na Alexandra Anord.

KUMBE KIRAKA

Kama ulihisi Kibwana ana uwezo wa kucheza beki pekee, achana na mawazo hayo anasema ana uwezo wa kucheza hadi winga tena bila wasiwasi wowote.

“Naweza kucheza kiungo wa pembeni, pia namba 2, 3 hata hizo namba za pembeni nacheza zote 7, 11,” anasema na kudokeza kwa miaka sita aliyoanza kucheza soka la ushindani, hajawahi kupewa kadi nyekundu kwa kuwa ni mchezaji anayezingatia sana nidhamu uwanjani.

“Nakumbuka nilipewa wakati nikiwa ‘Moro Youth’ katika mechi za kuwania jezi, na ni hiyo hiyo moja, sijawahi kupewa tena kwa miaka sita ya kucheza ligi za ushindani na timu ya taifa.”

BABA KUMBE YANGA

Anasema baba yake alisoma Shule ya Kibasila na alicheza Yanga B akikipiga Na.10 miaka ya nyuma hapo alipochaguliwa kupandishwa, lakini babake akapata matatizo ambayo hakutaka kumuweka wazi ni yapi ambayo yalimwamisha.

Advertisement