Kiburi cha Simba Dodoma hiki hapa

UIMARA wa safu ya ulinzi ya JKT Tanzania ndio kitu pekee kinachoweza kuibeba timu hiyo leo wakati watakapoialika Simba katika mechi ya raundi ya tano ya Ligi Kuu itakayochezwa Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.

Lakini Simba wana kiburi kutokana na makali ya safu ya ushambuliaji ambayo inailazimisha JKT Tanzania kucheza kwa umakini, tahadhari na nidhamu ya hali ya juu katika dakika 90 za mechi hiyo, vinginevyo inaweza kujikuta inapoteza pointi nyingine tatu baada ya kufungwa bao 1-0 katika mechi iliyopita ugenini na Coastal Union. Simba imepachika mabao 10 katika mechi nne za mwanzo dhidi ya Ihefu, Mtibwa Sugar, Biashara United na Gwambina FC.

Sio hilo tu bali pia safu ya ulinzi ya JKT Tanzania imekuwa na takwimu zisizoridhisha ambapo imeruhusu mabao manne katika mechi nne ilizocheza dhidi ya Kagera Sugar, Dodoma Jiji FC, Polisi Tanzania na Coastal Union.

Ukiondoa katika ulinzi, JKT Tanzania pia wanapaswa kuwa na makali katika kutumia nafasi za mabao ambazo wanatengeneza kwani wamekuwa na takwimu zisizoridhisha katika ufungaji, wakipachika mabao mawili tu katika mechi nne walizocheza huku wakitoka bila kufunga katika mechi mbili kati ya hizo.

Kiwango bora walichokionyesha katika mechi mbili zilizopita kikichagizwa na vita ya washambuliaji wake wanne Meddie Kagere, Chris Mugalu, Charles Ilanfya na John Bocco, ni jambo ambalo linatoa taswira ya ugumu ambao JKT Tanzania wanaweza kukutana nao.

Simba inaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kupata ushindi katika mechi ya mwisho iliyocheza Uwanja wa Jamhuri Dodoma ambao iliibuka na ushindi wa mabao 2-1 katika Fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam dhidi ya Mbao FC.

Mara nyingi JKT Tanzania imekuwa mnyonge mbele ya Simba, lakini kuna nyakati imekuwa ikiwashangaza kwa kuibuka na ushindi ama sare kama ilivyokuwa katika mchezo wa mzunguko wa pili msimu uliopita ambapo iliibuka na ushindi wa bao 1-0 uliochezwa Februari 7, 2020 katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Kiujumla, katika mechi 10 za mwisho kukutanisha timu hizo katika Ligi Kuu, Simba imeibuka na ushindi mara saba, JKT Tanzania mara mbili huku mara moja ni sare. Katika mechi hizo, Simba imefunga mabao 14 huku JKT Tanzania ikipachika sita.

Lakini achana na takwimu hizo pindi timu hizo zikutanapo, Simba wanajivunia pia historia nzuri katika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma ambako wamekuwa wakiibuka na ushindi mara kwa mara pindi wanapocheza.

Kumbukumbu zinaonyesha katika mechi tisa za mwisho za mashindano ambazo wamecheza, wameibuka na ushindi mara saba, sare moja na kupoteza moja.

Simba katika mechi hizo tisa imepachika mabao 13 huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa mara sita.

Kocha wa JKT Tanzania, Mohammed Abdallah ‘Bares’ alisema wanatambua ubora na historia nzuri ya Simba dhidi yao na ubora wa wapinzani wao lakini hawako tayari itumike kama fimbo ya kuwachapia.

“Maandalizi kwa upande wetu yako vizuri na wachezaji wote wako katika hali nzuri kwa ajili ya mchezo huo. Tumejikita zaidi katika kujiimarisha na kuandaa mipango yetu ya kiufundi ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri katika mechi hiyo.

Kuhusu Simba wao wanajipanga kivyao hivyo kwa sasa siwezi kuwazungumzia na kikubwa ni sisi kujipanga ili tuwe bora tuweze kuwa bora na kupata ushindi. hayo ya historia na ubora wao hatuyapi nafasi kwa sasa,” alisema Bares.

Meneja wa Simba, Patrick Rweyemamu alisema kuwa wachezaji wa timu hiyo wanapaswa kuhakikisha wanaibuka na ushindi katika mchezo huo kwani hakuna sababu itakayoeleweka kutoka kwao ikiwa hawatapata ushindi.

“Tunaenda kucheza na JKT Tanzania katika Uwanja wa Jamhuri tukiwa tumejiandaa vizuri kuhakikisha tunaibuka na ushindi lakini suala la ubovu wa eneo la kuchezea sio la kulitumia kama utetezi hivyo wachezaji wanatakiwa kupambana ili tuweze kuibuka na ushindi

Tuna wachezaji 27 ambao wote wako fiti na watasafiri na kocha anaweza kumtumia yeyote kulingana na mipango na mahitaji yake, “ alisema Rweyemamu.

“Kubwa tunawaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi kutupa sapoti ili tuweze kuibuka na ushindi katika mchezo huo lakini kwa maana ya morali na hamasa viko juu na wachezaji wana hamu ya kuipatia timu ushindi.”