Kiboko wa Yanga! Kitenge aota ufungaji bora

Muktasari:

  • Mshambuliaji huyo Mrundi tangu alipoifunga Yanga mabao matatu ameshindwa kufunga katika mechi yoyote ya Ligi Kuu Bara.

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Stand United 'Chama la Wana', Alex Kitenge aliyefunga mabao matatu (3) amewaambia wale wanaodhani aliotea kuwafunga Yanga ‘hat trick’ watakuwa wamepotea njia,ila wasubirie kuona maajabu.

Tangu Kitenge awafunge Yanga, hajapata nafasi ya kucheza na nyavu tena, lakini yeye alijigamba na kwamba atafunga sana na mechi bado zipo nyingi, hivyo hana hofu ya kuingia kwenye kinyang'anyiro cha kuwania kiatu cha dhahabu kwa msimu huu.

"Bado nina imani kubwa ya kufunga hat trick nyingi na kuendelea kuzifumania nyavu kwenye ligi hii ya Tanzania, najiamini mwisho wa msimu naweza kutwaa kiatu ama kuwa miongoni mwa wafungaji bora.

"Alianza kuongoza Meddie Kagere na sasa Eliud Ambokile kwa mabao sita, huenda siku zinazokuja nikawa mimi, nafasi ipo wazi kwa kila straika kujituma kwa bidii kujiweka kwenye mazingira mazuri ya kinyang'anyiro," alisema.

Alizungumzia ligi hiyo alisema ameona chipukizi wanaonyesha viwango vya hali ya juu na kwamba wakijituma kwa bidii anaamini watafika mbali.

"Kikubwa wawe wanajaribu kufikiria mbali kwa maana ya kukubali kujaribu changamoto za kuishi nje ya mipaka yao kama tulivyo sisi, kuacha soka la Burundi na kucheza Tanzania," alisema Kitenge.