Kibadeni: Wala sio Wambura ni Phiri aliyeichongea Serengeti Boys

Muktasari:

  • Serengeti waliifunga Zambia ya kocha Phiri aliyewahi kuifundisha Simba kwa nyakati tofauti ambaye alishangazwa kuona Nurdin Bakari akiwa kikosini huku akiwa ametoka kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.

Dar es Salaam. Nyota wa zamani wa kimataifa na kocha maarufu nchini, Abdallah KIbadeni 'King' alifichua ishu nzima ya na baba yake Mbwana Samatta sambamba na kufichua vitega uchumi vyake.

Pia aliwataja kina Jonas Mkude na urafiki wake na baba wa Msemaji wa Simba, Haji Manara, Sunday Manara 'Computer', nyota wa kimataifa wa Tanzania na Yanga sambamba na kueleza umuhimu wa watu wa saikolojia ndani ya timu za soka.

Katika kuhitimisha makala ya gwiji huyu anayeshikilia rekodi ya kufunga hat trick katika mechi ya watani wa jadi nchini Simba na Yanga mwaka 1977, Kibadeni anafichua mkasa mzima wa kuenguliwa kwa Serengeti Boys baada ya kufuzu Fainali za Afrika kwa Vijana U17 mwaka 2005.

Wakati timu hiyo ya taifa ya Vijana U17, Kibadeni ndiye aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu hiyo, lakini furaha yake ya kuipeleka timu hiyo katika fainali hizo kwa mara ya kwanza ziliishia hewani kabla ya Tanzania kufungiwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) kwa udanganyifu. Ilikuwaje? Endelea naye...!

PHIRI NDIYE ALIYEICHONGEA SERENGETI

Baada ya kufabnya vyema kwenye mechi za mchujo za kwenda Gambia, timu ya taifa ya vijana U17 Serengeti Boys ilijikuta ikiondolewa michuanoni baada ya kubainika imemchezesha mchezaji aiyestahili kushiriki michuano hiyo.

Ndio, mchezaji huyo aliyeiponza Serengeti alikuwa ni kiraka Nurdin Bakar ambaye pia alikuwa akiichezea Simba katika Ligi ya Mabingwa Afrika iking'olewa na Zanaco ya Zambia katika hatua ya awali.

Serengeti Boys baada ya kuzinyoosha na kuziondosha Rwanda kwa kuwanyuka mabao 2-1, Zambia kwa kuwafumua mabao 4-1 kisha kuinyoa Zimbabwe kwa 4-1, timu ilifuzu kwenda kwenda Gambia waliokuwa wenyeji na mabingwa wa mashindano ya mwaka huo.

Hata hivyo siku chache baada ya Zimbabwe kupigwa bao 1-0 baada ya kipigo cha mabao 3-1 ugenini walikata rufaa na kushinda na kuiponza Tanzania kuadhibiwa, KIbadeni anakumbuka mkasa huo na kusema; "Aliyetuchongea na Kocha Patrick Phiri aliyekuwa akiinoa timu ya Zambia na kuwatoa katika raundi ya kwanza."

Anasema Serengeti waliifunga Zambia ya kocha Phiri aliyewahi kuifundisha Simba kwa nyakati tofauti ambaye alishangazwa kuona Nurdin Bakari akiwa kikosini huku akiwa ametoka kucheza Ligi ya Mabingwa Afrika.

"Unajua watu wengi wanamlaumu Michael Wambura, hawajui ukweli, tukio hilo nililishuhudia mwenyewe kwa sababu nilikuwa na kikosi hicho, Nurdin alikuwa na miaka chini ya 17, akitokea timu ya Arusha, kiwango chake kiliwavutia matajiri wa Simba wakamchukua na kumsainisha kwa kumuongezea miaka.

"Serengeti wanatumia pasipoti, lakini Ligi ya Mabingwa timu zinatumia Leseni, Phiri alienda kuliambia shirikisho la kwao (Zambia) kwamba Nurdin kafoji umri ndipo CAF ikatuondoa kwenye mashindano hayo," anasema.

Anasema kitendo kile kiliwaumiza wachezaji na hata watanzania kwani zilitumika nguvu kubwa kukata tiketi ya kwenda Gambia ambayo mwishowe ilihamia kwa Zimbabwe ambao hata hivyo walienda kuchemsha kwa kucheza mechi zao za Kundi B bila kuambulia pointi hata moja.

TUZO TANO ZA UFUNGAJI BORA

Miaka aliyocheza ligi, King Mputa anasema amefanikiwa kunyakua tuzo za Mfungaji Bora mara tano, akidai zamani walikuwa wanapewa vikombe tofauti na sasa ni kiatu cha dhahabu kinachoambatanishwa na pesa.

"Vikombe hivyo nimevipeleka Chanika ambako kuna kituo changu cha soka, lengo nikuwapa moyo vijana kuamini katika nguvu zao ndio mafanikio yao," anasema.

UJAMAA UNAZITESA SIMBA, YANGA

Kibadeni anafichua kuwa, imekuwa ngumu Simba, Yanga na Taifa Stars kufika mbali kwenye michuano ya kimataifa akitaja sababu kuwa ni mfumo wa nchi uliokuwa unaendeshwa kijamaa unaowafanya wachezaji na viongozi kuwa wakarimu kwa wageni.

Kibadeni anasema alianza kuichezea Stars mwaka 1971 hadi 1978, anadai walikuwa wanaongozwa na ujamaa ambao ndio ulikuwa mfumo wa nchi.

"Mfano mzuri baba yangu alikataa ofa niliyokuwa nimeipata kwenda Yanga kisa akinitaka niwe mjamaa na Simba, lakini pia hakuniruhusu kwenda nje ambako nilikuwa natafutwa na timu nyingi aliniambia nilitumikie taifa na sio nchi za watu.

"Ndivyo ilivyokuwa zamani kwamba tukienda kucheza na nchi nyingine iwe kwenye timu ya taifa ama klabu, tuliambia tuonyeshe ujamaa ili kulitangaza taifa la Tanzania kwa sifa njema.

"Ajabu tulikuwa tukienda kwao, walikuwa hawatupokei vizuri mnaweza mkapewa hoteli ya ovyo ama vyakula vibaya ilimradi mtoke mchezoni, lakini walikuwa wakija huku tunawapokea kwa furaha na ukarimu mwingi, hilo ndilo linalowagharimu mpaka sasa," anasema.

NENO LAKE KWA SERIKALI

Kibadeni ameiomba serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, inayoongozwa na Rais John Magufuli, kuwatazama wastaafu waliofanya kazi ya kuweka misingi imara ya soka ambalo limeajiri vijana wengi, kuwapachika kwenye nafasi mbalimbali serikalini.

"Tunaona wenzetu waliostaafu serikalini na hata wanasiasa wanapewa heshima, iwe hivyo hata kwenye soka ujana wetu tukiwa na nguvu tumetumia huko, mfano mimi nimekuwa nikisoma, nimeenda nchi mbalimbali kwenda kusomea ukocha ikiwemo Brazil, kwa nini nisipewa nafasi hata Stars.

"Nimeanza kusomea mambo ya ukocha tangu mwaka 1980, nimesoma na mambo ya saikolojia, sema soka letu halijali watu wanaojua, mfano kwenye hizi timu zetu meneja anapaswa kuwa mtu wa mpira kocha akikwama anatoa ushauri wanawaweka watu wasioelewa kitu," anasema.

ATUNDIKA DARUGA

KIbadeni anasema baada ya kucheza soka kwa miaka 14 mfululizo kuanzia mwaka 1970 aliamua kustaafu kwa kutundika daruga zake mwaka 1984.

Anasema aliamua kuwapisha vijana na kujikita kwenye masuala ya ukocha aliokuwa ameshaanza kuusomea mapema enzi akiicheza.

Kibadeni anasema katika safari yake ya ukocha anajivunia mafanikio mbalimbali ikiwamo kuifikisha Simba katika Fainali za Kombe la CAF 1993 mbali na kutwaa mataji kadhaa katika timu alizowahi kuzionoa.

Baadhi ya timu ambazo zimeonja ujuzi wa kocha huyo ni pamoja na Majimaji, Simba, Kagera Sugar, Moro United, Taifa Stars, Serengeti Boys, Kilimanjaro Stars na nyingine, kitu anachojivunia.