Kiba soka anajua bwana!

Monday December 10 2018

 

By Burhan Yakub

Tanga.COASTAL Union jana Jumapili ililazimishwa sare nyumbani na Mbeya City, lakini kama kuna kitu kilichowafurahisha mashabiki wake, basi ni kucheza kwa mara ya kwanza kwa staa wao mpya, Ali Kiba aliyeupiga mwingi kwenye Uwanja wa Mkwakani, jijini hapa.

Kiba aliyecheza kwa muda wa dakika 64 kabla ya kutolewa alionyesha kiwango cha hali ya juu licha ya kuwa ni mara yake ya kwanza kucheza mechi ya Ligi Kuu Bara, huku akisababisha bao la kuongoza la timu yake lililofungwa dakika ya tano tu.

Staa huyo wa muziki wa kizazi kipya alikuwa hajaichezea Coastal tangu asajiliwe msimu huu, lakini jana Kocha Juma Mgunda alimuanzisha na kuzua sekeseke iliyozaa kona dakika ya tano ilitumbukizwa wavuni na Ayoub Lyanga.

Mara baada ya mchezo huo, Kiba alisema kiu yake ilikuwa ni kufunga bao, lakini alipoteza nafasi kadhaa na kudai anaamini kadri akipewa nafasi atafanya makubwa kuliko alichokionyesha katika mechi hiyo ambayo beki, Bakar Mwamnyeto wa Coastal alijifunga na kuipa sare City.

Sare hiyo imezifanya timu hizo kila moja kufika pointi 23, wakiikamata Mtibwa Sugar iliyopo nafasi ya nne, City ikifuata nyuma yao kwa uwiano wa mabao ya kufunga na kufungwa na Wagosi wa Kaya kusalia nafasi ya sita katika msimamo.

Advertisement