Kessy awakosa Senegal Afcon,kocha afunguka

Muktasari:

  • Hata hivyo kocha msaidizi wa Stars, Hemed Morocco alisema benchi la ufundi la timu hiyo halina presha yoyote kwa taarifa hiyo kwa sababu wachezaji wote waliowaita wana ubora wa kushiriki mashindano hayo.

BEKI wa kulia wa Timu ya Taifa ‘Taifa Stars’, Hassan Kessy atakosa mchezo wa kwanza wa mashindano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka huu huko Misri dhidi ya Senegal, Juni 23, kutokana na adhabu ya kutumikia kadi mbili za njano alizopata kwenye mechi za kuwania kufuzu fainali hizo.

Kessy alionyeshwa kadi hizo za njano kwenye mechi dhidi ya Cape Verde iliyochezwa Oktoba 12, 2018 ugenini huko Cape Verde ambayo Stars ilichapwa mabao 3-0 na ule wa mwisho dhidi ya Uganda uliochezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Machi 24, mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF) kwenda kwa Shirikisho la Mpira Tanzania (TFF), Kessy ndiye mchezaji pekee atakayekosa mchezo huo ingawa wengine wote wataweza kuwamo ikiwa watajumuishwa kwenye kikosi cha mwisho cha wachezaji 23.

Hata hivyo kocha msaidizi wa Stars, Hemed Morocco alisema benchi la ufundi la timu hiyo halina presha yoyote kwa taarifa hiyo kwa sababu wachezaji wote waliowaita wana ubora wa kushiriki mashindano hayo.

“Ni jambo la kawaida na linaweza kutokea hata kule kwenye mashindano, tunaweza tukawakosa wachezaji wengine lakini kwa upande wetu tunaamini hiyo itakuwa pia ni fursa kwa wachezaji wengine kuonyesha viwango na ubora.

“Tuna kikosi cha awali cha wachezaji 39 ambao yeyote anaweza kupata nafasi na akafanya vizuri hivyo hilo jambo halitupi wasiwasi,” alisema Morocco.

Wakati Stars ikijiandaa kumkosa Kessy kwenye mchezo wa ufunguzi, Senegal wenyewe watamkosa mshambuliaji wao nyota na tegemeo, Sadio Mane anayechezea Liverpool ambaye naye atatumikia adhabu ya kukosa mchezo mmoja baada ya kupata kadi mbili kwenye mashindano ya kufuzu.