Kessy ana yake kule Zambia

Monday August 6 2018

 

By CHARITY JAMES

BEKI wa kimataifa wa Tanzania aliyetua Nkana Red Devils ya Zambia, Hassan Kessy, amesema ametua klabuni hapo ili kupiga kazi ya kuipa mafanikio timu hiyo sambamba na kuendelea kupata nafasi timu ya taifa, Taifa Stars.

Stars mwezi ujao inatarajiwa kuvaana na Uganda katika mechi ya kuwania kufuzu fainali za Afcon 2019 zitakazofanyika Cameroon na Kessy ana kiu ya kuona anaingia kwenye kikosi kwa ajili ya mchezo huo.

Kessy alisaini mkataba wa miaka miwili akitokea Yanga aliyomaliza mkataba baada ya kuitumikia kwa misimu miwili na kudai kuwa ameenda Zambia kucheza soka na kiu yake ni kuona anafika mbali.

Nkana ipo nafasi ya tano kwenye Ligi Kuu Zambia ikiwa na alama 43, pointi 19 nyuma ya vinara Zesco inayonolewa na kocha wa zamani wa Yanga, George Lwandamina na Kessy alisema ana matumaini ya kucheza michezo 13 iliyosailia kama kocha wake atampa nafasi na amesema hatafanya makosa.

“Sipo tayari kufanya makosa katika mchezo wangu wa kwanza endapo nitapata nafasi ya kucheza mashabiki wangu wategemee mazuri kwani napambana kupata nafasi na kuwa miongoni mwa nyota wake wanaocheza kikosi cha kwanza,” alisema.

Advertisement