Kessy aitumia salam Simba ya Mo Dewji

Monday December 10 2018

 

By Eliya Solomon

BEKI wa kulia wa Nkana FC, Hassan Kessy ameitumia salamu timu yake ya zamani, Simba ambao atakutana nayo kwenye mchezo wa raundi ya kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

Kessy ameikaribisha Simba SC Zambia kwa kusema anatakuwa adui yao na mara baada ya mchezo huo kumalizika atashikana mikono na Watanzania wenzake kama ishara ya kuonyesha mpira siyo vita endelevu ni mchezo wa dakika tisini tu.

“Tutakuwa nyumbani na uzuri ligi imemalizika kwa hiyo mawazo yetu ni kwenye huo mchezo, binafsi naifahamu Simba kwa sababu nimeichezea na nimecheza dhidi yao pia mara kadhaa nimepata muda wa kuwaangalia nikiwa huko nyumbani.

“Siwezi kuwaongelea sana ila naona utakuwa mchezo mgumu ambao tumejiandaa nao kuhakikisha tunaanza vizuri hasa kwenye uwanja wetu wa nyumbani ili tusiwe na kazi kubwa ya kufanya ugenini,” alisema Kessy.

Beki huyo wa pembeni alisema hakuna mshambuliaji wa Simba anayemhofia kumdhibiti kwenye mchezo wa kwanza ambao Nkana itakuwa nyumbani kwenye uwanja wake uliopo Kitwe wenye uwezo wa kuingiza watazamaji 10,000 kabla ya kurudiana jijini Dar.

Advertisement