Kessy, Mpepo uso kwa uso Zambia

Muktasari:

  • Akizungumzia mfumo huo, Mpepo alisema ni mzuri na amedai utatoa nafasi kubwa ya kupigania kumaliza kwenye nafasi za juu zitakazowafanya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

ZAMBIA imeamua kubadili mfumo wa Ligi Kuu yao kwa kugawa makundi mawili ya timu ambazo zitacheza kwa kanda kabla ya vinara kuonyeshana ubabe kwenye mchezo wa kuwania ubingwa wa MTN Super Ligi.

Shirikisho la soka la Zambia (FAZ), limeamua kufanya mabadiliko hayo ya mfumo wa MTN Super Ligi kwa kuwa na kanda mbili ya Kaskazini na Kusini ili kuendana na kalenda mpya ya CAF.

Katika mfumo huo, Nkana ya Hassan Kessy itakuwa kwenye Ukanda wa Kaskazini pamoja na Green Eagles, Power Dynamos, Buildcon, Nkwazi, Forest Rangers, Napsa Stars, Lumwana Radiants na timu mbili zilizopanda daraja.

Katika mfumo huo, Kessy atakuna na Mtanzania mwenzake, Eliuter Mpepo ambaye wiki kadhaa nyuma alijiunga na Buildcon kwa kusaini mkataba wa miezi sita akitokea Singida United.

Akizungumzia mfumo huo, Mpepo alisema ni mzuri na amedai utatoa nafasi kubwa ya kupigania kumaliza kwenye nafasi za juu zitakazowafanya kushiriki michuano ya kimataifa msimu ujao.

“Timu ambayo itakuwa imekusanya pointi nyingi itacheza Ligi ya Mabingwa Afrika, nyingine mbili ambazo zitakuwa zinafuatia zinapata nafasi ya kushiriki Kombe la Shirikisho,” alisema Mpepo.

Kanda ya Kusini yenyewe ina Zesco United, Green Buffaloes, Zanaco, Kabwe Warriors, Red Arrows, Lusaka Dynamos, Kitwe United. Nakambala Leopards na timu mbili zilizopanda daraja.