Kesi ya akina Aveva kuanza kusikilizwa

Muktasari:

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili Simba, Zacharia Hans Poppe kwa upande wake amekiri kuhusika kwenye mchakato wa ununuzi wa nyasi za bandia, lakini washtakiwa wenzake wamekana mashitaka.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, kesho Jumatano itaanza kusikiliza ushahidi wa upande wa mashtaka katika kesi ya kughushi na kutakatisha fedha inayowakabili viongozi watatu wa Klabu wa Simba.
Washtakiwa hao ni Rais wa Klabu hiyo, Evans Aveva, makamu wake, Geofrey Nyange maarufu Kaburu na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe.
Hatua hiyo inatokana na upande wa mashtaka kumaliza kuwasomewa maelezo ya awali (PH) na hivyo, Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama hiyo, Thomas Simba, kupanga Oktoba 31,  2018 kuanza kisikiliza ushahidi.
Kesi hiyo inatokana na matumizi ya pesa za uhamisho wa mchezaji wa klabu hiyo, Emmanuel Okwi, kwenda Klabu ya Etoile Sportive Du Dahel ya Tunisia, kwa madai ya kutumia pesa hizo kununulia nyasi bandia na gharama za ujenzi wa uwanja huo.
Katika kesi hiyo Hans Poppe anakabiliwa na mashtaka mawili, kughushi nyaraka na kuwasilisha nyaraka za uongo yeye pamoja na wenzake.
Wakati, Avena na Nyange wanakabiliwa na mashtaka 10 yakiwemo matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha hizo bila mamlaka ya Kamati ya Utendaji ya Simba, kujipatia pesa isivyo halali (Aveva) na utakatishaji fedha.
Washtakiwa Aveva na Nyange wanatetewa na mawakili Nehemia Nkoko na Nestory Wandiba wakati Hans Poppe anatetewa wa Wakili Agostino Shio.
Siku waliposomewa maelezo ya awali,  Oktoba 19, 2018, mfanyabiashara Hans Poppe, alikiri mahakamani hapo kuhusika na mchakato wa ununuzi wa nyasi bandia kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa klabu hiyo, ulioko Bunju, wilaya ya Kinondoni,  wakati wenzake walikana mashtaka yao yote.
Katika hatua nyingine, kesi ya kula njama, kughushi na kutakatisha fedha inayomkabili aliyekuwa rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) Jamal Malinzi na wenzake wa wanne, inatarajia kuendelea na ushahidi.
Kes hiyo jinai namba 213/ 2017 inatarajia kuendelea kesho Jumatano Oktoba 31,  2018, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mbali na Malinzi(57), washtakiwa wengine  ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Joas Selestine (46) na Mhasibu wa TFF,  Nsiande Isawayo Mwanga (27).
Wengine, Meneja wa  Ofisi za TFF, Miriam  Zayumba na Karani wa TFF,  Flora Rauya ambao kwa pamoja  wanakabiliwa na mashtaka 30 katika kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa USD 173,335 na Sh 43,100,000.
Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji fedha kuwa miongoni mwa mashtaka  ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana huku wenzao Zayumba na Frola wapo nje kwa dhamana.
Tayari mashahidi nane upande wa mashtaka wametoa ushahidi  wao dhidi ya washtakiwa hao.