Kesi ya Aveva yakwama, shahidi mgonjwa

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi katika kesi inayowakabili vigogo watatu wa klabu ya Simba baada ya shahidi waliokuwa wanmtegemea kuugua na kushindwa kufika mahakamani hapo.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeshindwa kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi katika kesi inayowakabili vigogo watatu wa klabu ya Simba baada ya shahidi waliokuwa wanamtegemea kuugua na kushindwa kufika mahakamani hapo.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni aliyekuwa Rais wa Klabu hiyo, Evans Aveva, Makamu wa wake, Geofrey Nyange na Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu ya Simba, Zacharia Hans Poppe.
Wakili wa Takukuru, Leonard Swai alidai mahakamani hapo hawana shahidi na shauri hilo lilikuja kwa ajili ya kusikilizwa.
"Shauri lilikuja kwa ajili ya kusikiliza ushahidi hatuna shahidi ni mgonjwa, leo (Ijumaa) asubuhi amenipigia simu hivyo naiomba mahakama ipange Juni26, 2019 ili shauri lijalo nitakuja na mashahidi wawili,"alida Swai.
Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi, Janeth Mtega alisema upande wa mashtaka wanatakiwa kuwapelekea wito mashahidi hao ili wafike mahakamani hapo kwa ajili ya kutoa ushahidi.
Mtega aliahirisha shauri hilo hadi Juni 26, 2019 itakapokuja kwa ajili ya kusikiliza ushahidi.
Katika kesi ya msingi washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 10 ikiwemo kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi, kutoa maelezo ya uongo na utakatishaji wa fedha.
Katika shitaka la utakatishaji fedha linalomkabili Aveva, inadaiwa Machi 15, 2016 katika benki ya Baclays Mikocheni, Dar es Salaam alijipatia Dola za Kimarekani 187,817, takriban Sh. 400 milioni kutoka klabu hiyo wakati akijua zimetokana na zao la kosa la kughushi.
Shitaka lingine la kughushi linawakabili washtakiwa wote, ambapo wanadaiwa katika tarehe hizo hizo kwa pamoja walighushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zina thamani ya dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh. 90 miloni huku wakijua kwamba sio kweli.
Shitaka lingine inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya March10 na September 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.
Imeandaliwa na Pamela Chilongola, Daniel Francis na Sifras Kingamkono