Kesi Malinzi: Mashahidi waitwa Ikulu, wakwamisha kesi

Muktasari:

Kesi inayomkabili, aliyekuwa rais wa TFF, Jamal Malinzi na wenzake wa wanne itaendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ushahidi wa mashahidi wa upande wa mashtaka Oktoba 31 na Novemba Mosi mwaka huu.

Dar es Salaam. Kesi ya kula njama na kughushi, inayomkabili aliyekuwa rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Jamal Malinzi na wenzake wa wanne imeshindwa kuendelea kusikilizwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya mashahidi kuitwa ghafla Ikulu na Rais Dk. John Magufuli.

Hayo yameelezwa jana na  Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri, wakati wa kesi hilo ilipokuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji wa ushahidi upande wa jamhuri.

Hii ni mara ya pili, kwa kesi hiyo kuahirishwa mwezi huu, ikiwa katika hatua ya usikilizwaji.

Oktoba 16, mwaka huu, kesi hiyo iliahirishwa baada ya wakili Kimaro kuiomba mahakama hiyo, apitie mwenendo wa kesi hiyo kwa sababu ilikuwa inaendesha na wakili mwingine Leonard Swai, kutoka Takukuru,

Kimaro alidai mashahidi ambao alikuwa anawategemea kufika kwa ajili ya kutoa ushahidi wameitwa Ikulu, ghafla na Rais John Magufuli.

"Kesi ilikuja kwa ajili ya kuendelea na usikilizwaji na mashahidi ambao tulishaandaa wameitwa ghafla na Rais Magufuli Ikulu hivyo tunaomba tarehe nyingine ili tuweze kuendelea," amedai Kimaro.

Hata hivyo, upande wa mashtaka baada ya kuwasilisha hoja hizo, Wakili utetezi Richard Rweyongeza, alidai kwamba hoja ambazo zimetolewa na Wakili Kimaro zinaonyesha ni dharau kwa sababu kesi hiyo ina mashahidi wengi, ambao sio wote waliitwa Ikulu.

"Naomba upande wa mashitaka wajitahidi kutuletea mashahidi wa kutosha ili kesi iweze kuendelea kuliko kusubiri mashahidi hao tu, amedai.

Hakimu Mashauri baada ya kusikiliza hoja za pande mbili, aliwaagiza upande wa mashtaka kuleta mashahidi wa kutosha tarehe ijayo ili kesi iweze kuendelea.

Hakimu Mashauri aliahirisha shauri hilo hadi Oktoba 30 na Novemba mosi mwaka huu, kesi hiyo itakapoendelea na usikilizwaji ushahidi.

Mbali na  Malinzi(57),  washtakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa TFF, Mwesigwa Joas Selestine(46) na Mhasibu wa TFF,  Nsiande Isawayo Mwanga(27).

Wengine,  Meneja wa Ofisi ya TFF, Miriam Zayumba na Karani wa TFF, Flora Rauya ambao Kwa pamoja  wanakabiliwa na mashtaka 30 katika  kesi ya jinai namba 213 ya mwaka 2017 yakiwamo ya kula njama, kughushi, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na utakatishaji wa fedha wa USD 173,335 na Sh 43,100,000.

Malinzi, Mwesigwa na Nsiande wapo rumande kwa kukabiliwa na mashtaka ya utakatishaji wa fedha kuwa miongoni mwa mashtaka  ambayo kwa mujibu wa sheria hayana dhamana huku wenzao Zayumba na Frola wapo nje kwa dhamana.

Katika kesi hiyo tayari mashahidi nane wa upande wa mashtaka wamekwishatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.