Kerr aipa ushindi Kogalo kwa Ingwe

Muktasari:

Kerr aliyeipatia Gor ubingwa mara mbili kabla ya kusepa zake mwaka 2018 alisema ni lazima Gor itaichapa Ingwe, licha ya kukiri pambano hilo litakuwa gumu.

KOCHA wa zamani wa Simba, Dylan Kerr amebetia chama lake alilowahi kulinoa, Gor Mahia ‘K’Ogalo’ akidai lirashinda kwenye Mashemeji Derby dhidi ya wapinzani wao AFC Leopards maarufu kama Ingwe Jumapili hii kwenye Uwanja wa Moi Kasarani, mjini Nairobi nchini hapa.

Ingwe ambao ndio wenyeji wananolewa na Muingereza, Steven Polack, lakini Kerr ambaye naye ni raia wa Uingereza alisema anaamini Gor Mahia ndio yenye nafasi kubwa kuendeleza ubabe dhidi ya wapinzani kama ilivyokuwa kwenye derby yao ya kwanza walipowacharaza mabao 4-1.

Kerr aliyeipatia Gor ubingwa mara mbili kabla ya kusepa zake mwaka 2018 alisema ni lazima Gor itaichapa Ingwe, licha ya kukiri pambano hilo litakuwa gumu.

“Hilo halina ubishi. Ndio, Gor Mahia wanashinda mechi hii, sijui kwa mabao mangapi, ila hapa Ingwe hawatoki nakwambia, nimeimiss sana Mashemeji Derby, lakini niwatakie kila la heri katika mchezo wao,” alisema Kerr anayeinoa Baroka FC ya Afrika Kusini.

Msimu uliopita Gor Mahia iliitandika Ingwe mara mbili, baada ya kushinda raundi ya kwanza 2-0 na baadaye kumalizia kwa 3-1 waliporudiana na kwa sasa Gor inaongoza msimamo wa ligi ikiwa na pointi 51, huku Ingwe ikiwa katika nafasi ya sita na pointi 40.