Kenya U23 yatajwa, Mutamba ndani

Monday November 5 2018

 

By Fadhili Athumani

Nairobi, Kenya. Kocha wa timu ya taifa ya Kenya kwa vijana chini ya miaka 23, Francis KImanzi amekitaja kikosi cha mwisho kitakachoingia kambini kujiwinda na mchezo wa kusaka tiketi ya kufuzu michuano ya Kombe la Afrika (AFCON U23) dhidi ya Mauritania.

Katika kikosi hicho cha Emerging Stars cha wachezaji 18, wapo nyota kadhaa wa Harambee Stars wakiongozwa na Straika wa Sofapaka, Piston Mutamba, kipa wa Kariobangi Sharks, Brian Bwire na mwenzake Timothy Odhiambo kutoka Ulinzi Stars.

Kabla ya zoezi hilo lililofanyika ugani Moi Kasarani, jana jioni, kulikuwa na jumla ya wachezaji 57 ambapo baada ya mazoezi ya pamoja kwa siku mbili, hatimaye walipatikana nyota hao 18, zoezi ambalo Kocha Kimanzi, ambaye ni mmoja wa makocha wasaidizi wa Harambee Stars, alisema haikuwa rahisi kutokana na ushindani mkubwa ulio.

“Haikuwa kazi rahisi kuwapata hawa 18, kumbuka tulikuwa na siku mbili tu ya kuchagua kati ya wale 57. Vijana walionyesha ushindani mkubwa lakini, baada ya kuchuja kwa umakini, tulifanikiwa kukipata kikosi kitakachowavaa Mauritius. Shukrani kubwa kwa Sebastien Migne na msaidizi wake Nicolas Borrquet-Cor, walitusaidia sana,” alisema Kimanzi.

Emerging Stars, watacheza mechi mbili za kusaka tiketi ya kufuzu AFCON dhidi ya Mauritius. Mechi ya kwanza itapigwa Novemba 14, mwaka huu, ugani Moi Kasarani, Jijini Nairobi. Baada ya hapo watakutana na Sudan/Seychelles katika raundi ya pili.

Kikosi Kamili cha Emerging Stars

Makipa: Timothy Odhiambo (Ulinzi Stars) and Brian Bwire (Kariobangi Sharks)

Mabeki: Mike Kibwage (KCB), Lennox Ogutu (Mathare United), Johnstone Omurwa (Mathare United), David Owino (Mathare United), Harun Mwale (Ulinzi Stars) na Yusuf Mainge (AFC Leopards)

Viungo: Teddy Osok (Sofapaka), Tobias Otieno (Sony Sugar), Ibrahim  Shambi (Ulinzi Stars), Abdallah Ahmed (Mathare United), Chrispinus Onyango (KCB) na James Mazembe (Kariobangi Sharks)

Washambuliaji: Boniface Mukhekhe (Nakumatt), Piston Mutamba (Sofapaka), Sydney Lokale (Kariobangi Sharks) na Jeffary Owiti (AFC Leopards)

Advertisement