Kelvin John kumrithi Samatta Genk

Muktasari:

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Mbaki Mutahaba ambaye ni meneja wa mchezaji huyo alisema uongozi wa Genk umevutiwa na uwezo wa kijana huyo na kila kitu kuhusu makubaliano kimekamilika na kwamba kinachosubiriwa ni umri.

WAKATI Watanzania wengi wakisubiri kwa hamu kuona Mbwana Samatta akitangazwa rasmi kujiunga na Aston Villa inayoshiriki Ligi Kuu England, neema nyingine imeibuka.

Mshambuliaji chipukizi wa Tanzania, Kelvin John anajiunga rasmi na KRC Genk ya Ubelgiji ambayo nahodha huyo wa Taifa Stars alikuwa akiichezea.

Kelvin ambaye pia anaichezea timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20 ‘Ngorongoro Heroes’ amekamilisha dili hilo la kujiunga na Genk na kinachosubiriwa ni suala la umri tu.

Akizungumza na Mwanaspoti jana, Mbaki Mutahaba ambaye ni meneja wa mchezaji huyo alisema uongozi wa Genk umevutiwa na uwezo wa kijana huyo na kila kitu kuhusu makubaliano kimekamilika na kwamba kinachosubiriwa ni umri.

“Mwenyezi Mungu akijaalia atamrithi Samatta atakapofikisha umri wa miaka 18. Si mbali sana ni mapema mwakani kwa sasa bado anaendelea na masomo kwenye kituo cha Brooke House College Uingereza,” alisema.

“Hiyo ni kwa mujibu wa kanuni za kuingia na kukaa Ulaya hasa kutokana na udogo wa umri wake, imebidi aingie kama mwanafunzi na kuendelea kucheza soka kwenye kituo.”

Mutahaba alisema ni suala la muda tu kuona mchezaji huyo akikipiga kwenye timu hiyo kwani tayari alifanya majaribio na kikosi cha vijana sambamba na kupata muda wa kushiriki mazoezi na timu ya wakubwa.

Kelvin ambaye alijipatia umaarufu mkubwa nchini akiwa na timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’, aliwahi kufanya majaribio ya kujiunga na HB Køge ya Denmark.

Kinda huyo pia aliwahi kufanya majaribio na kufuzu kuchezea klabu ya Ajax Cape Town ya Afrika Kusini huku akitazamwa na kipa wa zamani wa Manchester United, Edwin van der Sar ambaye alikwenda huko kutokana na uhusiano uliopo baina ya Ajax ya Uholanzi ambayo alikuwa akiifanyia kazi.

Mratibu wa usimamizi wa vipaji katika klabu ya KRC Genk, Jos Daerden alionyesha kuvutiwa na kinda huyo alipokwenda Ubelgiji kwa ajili ya majaribio.