Kelele za Simba zabeba Kakolanya

Muktasari:

Kama mashabiki wa Simba wanadhani walimuumiza Kakolanya walipokuwa wanamzomea alipoumia kipindi cha pili walipocheza na Mbao FC, juzi Jumapili, Uwnaja wa Taifa basi wafahamu kuwa kipa huyo ndio ndio kwanza anaongeza juhudi za kufanya vizuri zaidi.

KIPA Mkongo Nkizi Kindoki ana kazi ngumu ya kuonyesha kiwango mbele ya Beno Kakolanya, aliyedai kelele za wapinzani wao wa Simba ndizo zinazomfanya afanye vizuri.
Kakolanya amekuwa kipenzi cha mashabiki kutokana na umahiri wake langoni akiwa amecheza mechi nne na kuruhusu bao moja, huku Kindoki akicheza mechi tatu ikiwamo ya juzi alipompokea kipa huyo aliyeumia, lakini akiruhusu mabao matatu.
Kakolanya, alisema zile kelele za mashabiki wa Simba dhidi ya Yanga na hata juzi walipomzomea alipoumia na kutolewa uwanjani, ndivyo vinavyompa hasira ya kufanya makubwa ili kuibeba timu yake.
"Kelele za Simba zimenipa nguvu ya kuendelea kulinda kiwango changu na kujituma kwa bidii kuhakikisha msimu huu naifanyia kitu klabu yangu, wajue tu kuzomea kwao hakuniumizi," alisema.
Kakolanya alisema anaendelea vizuri na jana Jumatatu alifanya mazoezi na timu ya taifa 'Taifa Stars' kabla ya usiku wa leo kupaa kuelekea Cape Verde katika mechi za kuwania Fainali za Afcon 2019, huku Andrew Vincent naye akisjisikilizia baada naye kuumia juzi.