Kazingua! Keane amchana Southgate kadi nyekundu ya Maguire

London, England. ACHANA na bao la mkwaju wa penalti la Christian Erikssen, huko England stori ya mjini ni Harry Maguire na kinda wa Chelsea, Reece James.

Maguire, ambaye ni nahodha wa Manchester United ni kama aliimaliza mechi ya Ligi ya Mataifa Ulaya kati ya timu ya Taifa ya England na Denmark baada ya kupewa kadi nyekundu dakika ya 31 tu.

Alianza kwa kupewa kadi ya pili ya njano kwenye mchezo ambao ulimshughudia Kocha Gareth Southgate akipoteza mchezo wa kwanza katika kipindi cha miezi 12 tena kwenye dimba la Wembley.

Kupoteza kwa mchezo huo kumeisukuma England hadi nafasi ya tatu kwenye msimamo ambao kwa sasa unaongozwa na Ubelgiji kisha Denmark na England inafuatia huku Iceland ikishika mkia.

England imeshinda mechi mbili, sare moja na kupoteza mmoja wakati Ubelgiji imeshinda zote na kupoteza moja dhidi ya England.

Hata hivyo, wakati mjadala mkubwa ni kuhusu kadi ya Maguire ya kipindi cha kwanza tofauti na James, ambaye ndio mchezo wake wa kwanza kuichezea Three Lions na kupigwa kadi nyekundu wakati mchezo ukiwa umemalizika kwa kumbughdhi mwamuzi.

Nahodha wa zamani wa Manchester United ambaye kwa sasa ni mchambuzi wa Sky Sport, Roy Keane amemponda Southgate kwa kuonyesha kitendo cha kumkatisha tamaa beki huyo aliyenaswa kwa dau la rekodi kutoka Leicester City kwenda Man United.

Baada ya kupewa kadi hiyo, Keane alisema Southgate alipaswa kuonyesha uungwana kwa kumtia moyo wakati akitoka uwanjani badala ya kumpotezea na kumuona kama mkosaji.

Keane, ambaye anafahamika kwa kuzungumza ukweli, alisema Maguire amekumbana na majanga mengi ndani na nje ya uwanja hivyo, kumuacha apambane mwenyewe ni kuendelea kumpoteza.

“Nadhani Gareth anafahamu nini kinaendelea kwa Harry, anapita kwenye kipindi kigumu sana kwa takribani wiki tatu sasa ndani na nje ya uwanja. Anastahili kusaidiwa na sio kupuuzwa kama ilivyofanyika wakati anatolewa nje kwa adhabu,” alisema Keane na kuongeza:

“Hata ukiangalia kinachoendelea kwa sasa ndani ya Man United utaona tatizo kubwa ni Maguire. Hayupo vizuri tangu aliporejea kikosini na amepoteza hali ya kujiamini. Aliwekwa mahabusu akiwa mapumzikoni kule Mykonos, sasa anakuwaje sawa huyu. ”

Lakini, Southgate amekiri kuwa kikosi chake kinapswa kujenga nidhamu kutokana na matukio ya Maguire na James ambao wote walipewa kadi nyekundi ikiwa ni mara ya kwanza kwa wachezaji wawili wa England kupewa kadi kwenye mchezo mmoja.

Pia, akaonya kuwa utovu wa nidhamu wa wachezaji wake unaweza kuwaponza wakashindwa kufikia malengo ya kubeba taji hilo la Mataifa Ulaya.

Katika mchezo huo, makosa ya kujichanganya katika kuokoa hatari ya kipa Jordan Pickford na beki wake Kyle Walker ndio yaliigharimu England baada ya Denmark kupata penalti iliyokwamishwa wavuni na Erikssen.

Southgate, anakabiliwa na wakati mgumu kutokana na kile kinachoelezwa kukithiri kwa matukio ya utovu wa nidhamu wa baadhi ya wachezaji wake.

Hivi karibuni baadhi ya wachezaji akiwemo makinda Mason Greenwood, Foden waliondolewa kwenye kikosi hicho baada ya kukaribisha wanawake kambini na kukiuka kanuni za kukabiliana na corona. Pia, Jadon Sancho naye alidaiwa kutoroka kambini kwenda kula bata.