Kaze awapiga benchi Kisinda na Kaseke, wakiivaa Biashara

Muktasari:

Kaze amepangua kikosi chake katika maeneo matatu kwa kuanzisha wachezaji tofauti na wale ambao wameanza katika mchezo uliopita.

KOCHA wa Yanga, Cedric Kaze amepangua kikosi chake kitakachoshuka dimbani leo kucheza dhidi ya Biashara United mchezo utakaochezwa saa 10:00 katika Uwanja wa Karume, Mara.

Kaze katika kikosi hiko amewaingiza Adeyum Saleh akichukua nafasi ya Yassin Mustafa, Ditram Nchimbi akichukua nafasi ya Tuisila Kisinda  na Farid Mussa akichukua nafasi ya Deus Kaseke ambao  wote walianza katika mchezo uliopita.

Mabadiliko hayo yanaonyesha dhahiri kwamba kocha Kaze anataka timu inayocheza kwa spidi kwani mawinga wote, Farid na Nchimbi huwa wanatumia nguvu na spidi katika kupeleka mashambulizi.

Katika kikosi hiko hakuna mabadiliko mengine yaliyofanyika zaidi ya nafasi hizo tatu ambazo amefanya leo hii.

Kikosi kinachoanza ni Metacha Mnata, Kibwana Shomari, Adeyum Saleh, Lamine Moro, Bakari Mwamnyeto, Tonombe Mukoko, Ditram Nchimbi, Fei Toto, Farid Mussa, Waziri Junior na Michael Sarpong.

Upande wa benchi ni Faruk Shikhalo, Abdallah Shaibu 'Ninja', Zawad Mauya, Deus Kaseke, Yassin Mustafa, Yacouba Sogne na Tuisila Kisinda.

BEI YA TIKETI YAPANDA GHAFLA

Mashabiki na wadau wa soka mjini hapa wameonekana kusikitishwa na viingilio vya mchezo huo kupaa ghafla tofauti na ilivyokuwa imepangwa awali.

Taarifa ilizopata Mwanaspoti uwanjani hapo ni kuwa viingilio katika mechi hiyo ilikuwa ni Sh 3,000 kwa watoto, 5,000 mzunguko na 20,000 jukwaa Kuu (V.I.P).

Mashabiki wameonekana kushtushwa na taarifa za ghafla kwa kuongeza gharama za viingilio kutoka Sh 5,000 hadi Sh 10,000 na kuwafanya baadhi ya wadau kuishia getini.

Shaban Hamis mmoja ya mashabiki wa soka waliokutana na kadhia hiyo, amesema yeye alikuja na bajeti yake ya Sh 5,000 lakini hatua ya kukuta mabadiliko imemfanya kuishia getini.

"Walitangaza viingilio vya Sh 3,000, 5,000 na 20,000 lakini wamebadilisha kwa 5,000 kufikia 10,000 hii inatufanya sisi wenye uwezo wa chini kukosa burudani" amesema Hamis.,

Uongozi wa Chama cha Soka Mkoa wa Mara (FAM) kupitia kwa Katibu Mkuu wake, Elias Silas amesema tayari wamerekebisha hali hiyo na kuweka viingilio vya awali.

"Hilo limeshafanyiwa kazi, tumerekebisha na sasa wanaingia kwa bei ile ile iliyotangazwa awali" amesema Silas.