Kaze awahisha dawa

Tuesday October 06 2020
kaze pic

NI rasmi kwamba Kocha Mrundi, Cedrick Kaze ndiye bosi mpya wa Yanga na atakuwepo kwenye benchi la ufundi katika mechi dhidi ya Simba, Oktoba 18.

Kocha huyo amewapagawisha zaidi mabosi wa Yanga baada ya kuwaambia kwamba, alikuwa akifuatilia kila kitu kwenye mechi za timu hiyo tangu ligi ianze na kuwatamkia mambo mawili;

“Timu ni nzuri inahitaji mabadiliko madogo ili kuifanya kuwa bora zaidi uwanjani. Nadhani hilo ni jambo ambalo linawezekana kufanyika ndani ya muda mfupi.”

Habari hizo zimewafurahisha vigogo wa Yanga ambao wanaamini ujio wa Kaze unaweza kubadili mambo uwanjani na kukata ngebe za Simba wanayokutana nayo Oktoba 18 katika mechi ya Ligi kwenye Uwanja wa Mkapa. Pia Kocha huyo amewaambia Yanga kwamba anajua kinachoendelea Simba na akikaa na vijana wake ndani ya muda mfupi kwa kuangalia pia video za Simba atawapa mbinu mbadala wala wasiwaze sana.

Rekodi za Simba ambayo imekuwa na uwezo mkubwa wa kufunga mabao mengi kutokana na makali ya safu yao ya ushambuliaji na kiungo, zimekuwa zikiwanyima raha Yanga ambao, ushindi wao mkubwa kwenye ligi ni mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union.

Kaze anakuja kuchukua nafasi ya Mserbia, Zlatko Krmpotic ambaye Yanga wamempiga chini baada ya kutoridhishwa na mbinu zake pamoja na udhaifu wa kiufundi ingawa Hersi Said wa Yanga amekuwa akifanya siri.

Advertisement

Mpaka sasa Mwanaspoti limejiridhisha kwamba Kaze, ambaye awali ndiye alipewa jukumu la kuja kuinoa Yanga kabla ya Zlatko kutua, lakini kutokana na sababu za kifamilia zilizohitaji muda mrefu kuzimaliza zikafuta dili hilo, amemalizana na mabosi wa Yanga.

Habari za kuaminika ni kwamba, kwa sasa Kaze anakamilisha vibali vyake muhimu ili kumuwezesha kuanza safari ya kutoka Canada kuja Bongo mwishoni mwa wiki ijayo.

Habari za uhakika kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Kaze amewaambia viongozi kuwa timu hiyo ni nzuri na ina uwezo wa kurekebishwa na ikacheza soka la kisasa na lenye kuwapa raha mashabiki kwa kuwa, kuna wachezaji wazuri na wenye vipaji.

Mmoja wa viongozi wa Yanga aliidokeza Mwanaspoti jana kwamba, wanaamini Kaze atatua nchini wikiendi ijayo kama alivyowahakikishia.

“Tumeshamalizana naye na tunatarajia wikiendi hii atatua nchini kwa sababu anachokifanya sasa ni kukamilisha mambo ya vibali vyake na taratibu za kiafya za kuondoka Canada kutokana na mambo ya corona,” alidokeza kiongozi huyo na kusisitiza wakishamaliza kila kitu watamtangaza rasmi.

Katika mechi tano Yanga ilizocheza kwenye Ligi Bara, imekusanya pointi 13 wakiwa wameruhusu bao moja tu. Katika mechi hizo wameshinda nne na sare moja, haijapoteza mchezo wakipachika mabao saba.

Kama Kaze akitua atakuwa na siku 7 tu mkononi kabla ya kuikabili Simba lakini wachambuzi wa soka wanampa msaidizi wake, Juma Mwambusi nafasi kubwa ya kuongoza shoo hiyo ingawa Kaze alihusika kwenye usajili wa wachezaji kadhaa wa Yanga.

 

Advertisement