Kaze atetea mipango yake, ataka kasi zaidi

Muktasari:

Kaze amefanikiwa kupata ushindi wa kwanza wa Ligi Kuu tangu alipochukua mikoba kuinoa miamba hiyo.

Dar es Salaam. Kiwango ambacho kocha Cedric Kaze anakitaka kuona nyota wake wakitandaza soka uwanjani kimeanza kuonekana licha ya kuwa na timu kwa siku tano kabla ya mchezo wa kwanza.

Licha ya kuwazia zaidi pointi tatu katika mchezo wake wa kwanza baada ya kuanza kuinoa Yanga, Kaze alitaka zaidi kuona mashambuliai yakianzia nyuma katika pasi za haraka na kuachia nafasi.

Akizitaja nafasi mbili za mashuti ya Feisal Salum, kocha huyo raia wa Burundi alisema ni wazi kuwa nyota wake wanafundishika na wameanza kuelewa nini anataka katika michezo yao ya sasa.

“Kiasi naweza kusema kimeanza kuonekana kile ambacho nakitaka, japo ni kweli kwamba sikutarajia kwa kikosi changu kucheza nitakavyo kwa asilimia 100.

“Tulifanikiwa kutengeneza nafasi za kufunga lakini hatukufanikiwa hasa kipindi cha kwanza, lakini bado hatujakuwa makini katika final third (eneo la mwisho la ushambuliaji),” alisema Kaze.

Akizungumzia suala la mabadiliko ya washambuliaji, kocha huyo kijana alisema aliamua kumwanzisha Yacouba Sogne kutokana na mazoezi waliyofanya.

Alisema alichogundua ni kutokuwa wabunifu zaidi katika kumaliza mechi mapema, kwani suala kubwa kwa sasa ni kuanza kushambulia kutokea nyuma kwa kupiga pasi nyingi.

“Tunafanya kazi kubwa kutoka nyuma kwa pasi, awali tulikuwa na aina ya kucheza mipira mirefu, kitu ambacho nimekikataza, ndiyo maana dhidi ya Polisi Tanzania tulijitahidi kuweka mpira chini.

“Kila mchezaji atapata nafasi ya kucheza na kuonyesha nini anajifunza kutoka mazoezini na naamini mabadiliko yatakuja, hii si kazi ya kulala na kuamka tu,” aliongeza.

Yanga inatarajia kuondoka dar es Salaam leo kwenda Mwanza kwa ajili ya mchezo wao wa kesho wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya KMC, utakaofanyika Uwanja wa CCM Kirumba.

Baada ya mchezo huo wa kesho, mabingwa hao wa zamani wa Tanzania Bara watakuwa na michezo mingine miwili Kanda ya Ziwa, dhidi ya Gwambina na Biashara United ya Mara.

Lakini leo, Ligi Kuu itaendelea kwa michezo mitatu. Ihefu FC itakuwa Uwanja wa Sokoine kucheza na Namungo, wakati Coastal Union wakiwa kwenye Uwanja wa CCM Mkwakwani jijini Tanga.

Mbeya City ikiwa chini ya kocha msaidizi, Mathias Wandiba itakuwa na nafasi ya kujiuliza ugenini itakapocheza na Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.