Kaze apewa jeshi 11 la ushindi, kutua kambini Jumatano

MWANASPOTI limejiridhisha kwamba, Kocha mpya wa Yanga, Cedric Kaze atakanyaga ardhi ya Dar es Salaam Jumatano mchana kuanza majukumu yake Jangwani, lakini takwimu za mechi tano zilizopita zimemuonyesha silaha za kikosi chake cha kwanza.

Hakuna shaka kuwa Kaze amekuwa akiwasiliana na benchi la ufundi la Yanga husa kocha wa makipa aliyemtanguliza, Vladmir Niyonkuru. Uamuzi wa Yanga kumchukua Kaze unaweza kugeuka shubiri, lakini pia ukawa na neema kwa baadhi ya wachezaji na wapo watakaojikuta wakisota benchi na watakaopata nafasi ya kucheza tofauti na ilivyokuwa chini ya Zlatko Krmpotic.

Tathmini ya Mwanaspoti imebaini nyota 11 wa Yanga ambao, huenda wakaunda kikosi cha kwanza chini ya Kaze ikiwa atapitia ripoti ya mechi nane ambazo timu hiyo imeshacheza mpaka sasa, kuanzia wakati wa maandalizi hadi sasa msimu ulipofikia raundi ya tano. Wachezaji hao 11 ndio wameonekana kuwa na nyota ya ushindi kwani katika idadi kubwa ya mechi ambazo wanakuwa uwanjani, Yanga inapata matokeo mazuri tofauti na kwa wengine.

Baadhi ya wachezaji wamekuwa ndio wabadilishaji wazuri wa matokeo, na waimarishaji wa timu pale inapokuwa haina mwelekeo wa kuibuka na ushindi hasa wakiingia kutokea benchi.

Hapana shaka upande wa langoni, Kaze ataendelea kumfanya Metacha Mnata kuwa chaguo la kwanza kutokana na rekodi ya kipa huyo kutoruhusu bao lolote katika mechi nne alizocheza katika Ligi Kuu, ingawa pia hajaruhusu bao katika mechi tatu za kirafiki dhidi ya Mlandege, KMKM na Aigle Noir ya Burundi ambazo kila moja alidaka kwa muda wa dakika 45.

Katika ukuta, mabeki watatu ambao ni Bakari Mwamnyeto, Yassin Mustafa na Lamine Moro wana nafasi ya kuendelea kuwa katika kikosi cha kwanza kwani, wamekuwepo mara nyingi kikosini pindi Yanga inapopata matokeo iwe kipindi cha kwanza au cha pili. Lakini, hali inaweza kuwa tete kwa Shomary Kibwana anayecheza upande wa beki wa kulia, ambaye hana nyota nzuri mbele ya Deus Kaseke ambaye ameshiriki mara sita katika kikosi ambacho kimeipatia ushindi mfano ikiwa ni mechi dhidi ya Coastal Union, ambapo aliingia katika muda ambao timu yake ilikuwa sare, lakini baadaye ikaweza kufunga mabao matatu.

Katika safu ya kiungo, ubunifu wa Haruna Niyonzima hasa katika mchezo dhidi ya Coastal Union ambao aliingia wakiwa hawajapata ushindi, unaweza kumpa nafasi ndani ya kikosi cha Kaze akicheza sambamba na Mukoko Tonombe na Feisal Salum (Fei Toto).

Tonombe alikuwepo kikosini muda ambao Yanga ilifunga bao pekee dhidi ya Mbeya City, akifunga bao pekee la ushindi dhidi ya Kagera Sugar, akawemo kwenye kikosi cha ushindi dhidi ya Mtibwa Sugar pale Morogoro, akafunga katika mechi ya kirafiki dhidi ya Mlandege na pia akacheza dhidi ya KMKM.

Katika safu ya ushambuliaji, Michael Sarpong bila shaka ataendelea kuwa chaguo la kwanza akicheza jirani ya lango la adui, lakini huenda akacheza mbele ya viungo Tuisila Kisinda na Carlos Carlinhos.

Carlinhos licha ya kutokea benchi kwenye baadhi ya mechi, alikuwemo katika kikosi cha Yanga kilichoshinda dhidi ya Coastal Union, Mbeya City, Kagera Sugar, Mtibwa Sugar, Mlandege na KMKM ambako kote amekuwa na mchango mkubwa.

Beki wa zamani wa Yanga, Bakari Malima alisema ana imani kubwa timu hiyo itakuwa tishio iwapo kocha ajaye ataweza kuwaunganisha vyema wachezaji waliopo.

“Yanga ya sasa ina wachezaji wazuri na wana uwezo binafsi, sasa akipatikana kocha ambaye atawaunganisha vyema, bila shaka itakuwa inapata matokeo mazuri na kucheza soka safi tofauti na ilipokuwa na mwalimu aliyeondolewa,” alisema Malima.

Makamu mwenyekiti wa kamati ya mashindano ya Yanga, Injinia Said Hersi alisema kuwa klabu hiyo ina imani kubwa na Kaze kuwa atawatengenezea timu bora na yenye ushindani.

“Tulimuondoa Zlatko kwa kuwa tulikuwa haturidhishwi na mpira wake, falsafa yake na mengine. Kwa sasa timu itakuwa chini ya Mwalimu Juma Mwambusi mpaka hapo kocha mpya atakapokuja na kukabidhiwa rasmi.

“Miongoni mwa wale ambao tumewapa kipaumbele ni pamoja na Kaze kwa kuwa alikuwa ni chaguo letu la kwanza mwanzo. Ila kwa sasa bado kuna mambo tunakamilisha yakiwa sawa mashabiki watajua,” alisema Hersi ni maarufu kwa mashabiki wa Yanga.

Kaze amewaambia viongozi wa Yanga kwamba timu hiyo ni nzuri ila inahitaji maelekezo mazuri tu.