Kaze abadili kikosi Yanga, Waziri asalia

Muktasari:

Mpaka sasa  wamecheza mechi nane na kushinda saba dhidi ya Mbeya City 1-0, Kagera Sugar 1-0, Mtibwa Sugar 1-0, Coastal Union 3-0, Polisi Tanzania 1-0, KMC 2-1, na Biashara United 1-0 huku akiwa ametoa sare moja dhidi ya Tanzania Prison 1-1.

Kuelekea mchezo wa Ligi Kuu Bara muda uchache ujao kati ya Gwambina na Yanga kocha mkuu wa Yanga Cedric Kaze amebadili jumla ya wachezaji nane.

Mshambuliaji Waziri Junior na Metacha Mnata ndio wachezaji pekee walioanza kwenye mechi iliyopita dhidi ya Biashara United na wameonekana kwenye kikosi cha kwanza cha leo dhidi ya Gwambina.

Kikosi cha leo ni Metacha Mnata, Paul Godfrey, Yassin Mustapher, Said Makapu, Abdallah Shaib, Zawad Mauya, Abdulaziz Makame, Tuisila Kisinda, Yocouba Sogne, Deus Kaseke na Wazir Junior.

Shomary Kibwana, Bakariu Nondo, Mukoko Tunombe, Ditram Nchimbi, Farid Mussa na Michael Sarpong ni wachezaji walioanza kwenye mchezo uliopita lakini leo wanmeonekana kuwa benchi.

huenda kaze amefanya hivyo ili kutunza siraha zake za kikosi cha kwanza kwa ajili ya mchezo wa Novemba 7 dhidi ya watani zao Simba SC.

Endapo Yanga atashinda mechi ya leo atafikisha pointi 12 na kupanda mpaka kileleni mwa msimamo wa ligi.

MASHABIKI MAPEMA TU

Mashabiki wa Yanga hawataki kupoteza muda inapokuja suala la kusapoti chama lao, kwani hadi sasa tayari wameshauteka uwanja wa Gwambina kuelekea mchezo huo.

Unaweza usiamini, lakini ukweli ni kuwa mashabiki wa Yanga wameonekana kuwafunika wapinzani wao kutokana na kujaza jukwaa lao mapema.

Kwa upande wa Gwambina bado sehemu yao ni nyeupe na hakuna shamra shamra kama ilivyo kwa 'Wananchi' ambao muda wote ni shangwe tu.

ZAHERA USO KWA USO NA YANGA

Wakati wadau wa soka wakiendelea kusubiri kwa hamu pambano la mechi hiyo, kazi kubwa leo itakuwa kwa aliyewahi kuwa Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera atakapowakabili mabosi wake wa zamani.

Tangu Yanga kuachana Zahera, leo ndio mara ya kwanza kukutana na waajili wake hao wa zamani katika mechi ya Ligi Kuu, ambapo kila mmoja atahitaji kuonesha ubabe kwa mwenzake.

Hata hivyo wakati wapinzani hao wakishuka dimbani, Yanga inajivunia rekodi ya ushindi walipokutana mara ya mwisho katika mchezo wa kombe la Shirikisho (ASFC) msimu uliopita kwa ushindi wa bao 1-0 mechi iliyopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.