Katibu aanza na majeruhi Yanga

Saturday November 9 2019

 

By Khatimu Naheka

KAIMU Katibu Mkuu wa Yanga, Thabity Bashiri amefanya vikao tofauti na wachezaji wa timu hiyo waliokuwa nje kwa majeruhi ya muda mrefu.
Bashiri amechukua hatua hiyo ikiwa ni mwanzo wa kutaka kujua hali za wachezaji hao ambao wamekaa nje kwa muda mrefu katika kikosi chao.
Kiongozi huyo alianza kukutana na beki wa kulia Paul Godfrey 'Boxer' aliyeumia katika mchezo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu wakati Yanga ikicheza na Township Rollers.
Mpaka sasa Boxer ambaye msimu uliopita alikuwa beki muhimu hajafanikiwa kurejea katika kikosi hicho ingawa inaelezwa ameanza mazoezi mepesi.
Mbali na Boxer, pia Bashiri amekutana na winga Juma Mahadh ambaye naye aliumia goti misimu miwili iliyopita ambaye naye ameanza mazoezi baada ya kufanyiwa upasuaji nchini India.
Pia, bosi huyo alimfuata mshambuliaji Mzambia Maybin Kalengo ambaye alivunjika mfupa jijini Mwanza wiki chache zilizopita akiendelea na matibabu.
Aidha katika taarifa ambayo Yanga imeitoa imeeleza kuwa  bosi huyo amewaambia wachezaji hao kuwa klabu yao itaendelea kufuatilia matibabu yao pamoja na kugharamia kila kitu kitakachokuwa kinahitajika.

Advertisement