Katiba Yanga yamuengua Manji madarakani

Muktasari:

Yanga inatakiwa kufanya uchaguzi Januari 13 na tayari fomu zinachukuliwa na mwisho ni Novemba 13

Dar es Salaam. Pamoja na Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini wa klabu ya Yanga, George Mkuchika kutangaza kurejea kwa mwenyekiti Yusuf Manji madarakani, lakini Katiba ya klabu hiyo inampinga.

Jana Jumapili, Mwenyekiti wa Bodi ya wadhamini wa Yanga, Mkuchika alitangaza uwepo wa Manji kuendelea kuwa Mwenyekiti wa klabu hiyo ikiwa ni siku chache baada ya Serikali kupitia Baraza la Michezo la Taifa (BMT) kuiagiza TFF kusimamia uchaguzi wa klabu hiyo Januari 13 mwakani.

Katiba ya Yanga Ibara ya 28 inamuondoa Manji kuendelea kuwa Mwenyekiti.

Kifungu cha (1) cha ibara hiyo kinasema kamati ya utendaji wa Yanga inaundwa na Mwenyekiti, Makamu mwenyekiti, wajumbe wanane wa kuchaguliwa na mkutano mkuu na wajumbe watano watakaoteuliwa na kamati tendaji, wawili kati yao watatoka Zanzibar.

Kifungu cha 3 kinasema mjumbe atakoma kuwa mjumbe wa kamati tendaji iwapo atatenda au kufanya yafuatayo

(a) kujiuzuru kwa maandishi na kuwasirisha barua yake ya kujiuzuru kwenye kamati tendaji, (b) hataudhuria mikutano minne mfululizo ya kawaida ya kamati kuu bila sababu za msingi

(c) Anashindwa kutekeleza majukumu ya mjumbe kutokana na kuumwa au sababu nyingine yoyote kwa kipindi cha miezi 12 mfululizo, (d) Anapatikana na kosa la jinai na kuhukumiwa kufungwa bila mbadala wa faini.

Tangu Mei mwaka 2017, Manji alijiondoa kujihusisha na masuala ya Yanga huku kukiwa na sintofahamu kama yupo au la hadi Jana ambapo Mkuchika alisema bado yupo na Mwenyekiti wa klabu hiyo kongwe.

Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya TFF, Wakili Ally Mchungahela amesisitiza kuwa uchaguzi wa Yanga huko pale pale na hawatambui kurejea kwa Manji huku Yanga ikisisitiza Mwenyekiti yupo.

Mchungahela alisema kuwa kama Yanga wanamhitaji Manji wamchukulie fomu ya kugombea wamchague upya, lakini wao hawatambui kurejea kwake.

“Serikali ilimuita, BMT pia ikamuita ili kujua hatma yake, TFF ikamuandikia barua hakujibu, baada ya kusikia uchaguzi umeitishwa ndipo anarejea, hatutambui kurejea kwake," alisisitiza.