Kasi yote ni kupata kiatu cha dhahabu

Muktasari:

  • Messi anaongoza kwa sasa akiwa na ameweka kambani mabao 21 huko kwenye La Liga na kila bao moja lina thamani ya pointi mbili, kwa Ligi Kuu tano bora za Ulaya, ikiwa ni La Liga, Ligi Kuu England, Bundesliga, Ligue 1 na Serie A. Kutokana na hilo, hivyo Messi atakuwa na pointi 42 kwenye mchekamchaka wa kuwania ufungaji bora wa Ulaya.

LONDON, ENGLAND.SUPASTAA, Lionel Messi yupo pale juu, lakini mpinzani wake wa siku nyingi, Cristiano Ronaldo anakuja kwa kasi kwelikweli.

Vita ni kubwa na mambo ni mengi, tatizo muda mchache.

Ronaldo akiwa ndani ya uzi wa Juventus alitupia dhidi ya Sassuolo na bao hilo limemfanya awe amezidiwa kwa mabao matatu tu dhidi ya Leo Messi na kufanya mbio za kufukuzia Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya kuwa kali na zenye mvuto mkubwa.

Supastaa huyo wa Ureno alifunga bao lake la tisa mfululizo katika mechi za ugenini akiwa na Juventus na hiyo ni rekodi ambayo hakuna mtu mwingine aliyewahi kuifikia zaidi ya Giuseppe Signori, aliyefanya hivyo miaka mingi iliyopita, mwaka 1993 huko, hata Anthony Martial alikuwa hajazaliwa.

Kinachonogesha mbio za kuwania Kiatu cha Dhahabu cha Ulaya ni mastaa wake wanaofukuzia tuzo hiyo ya ufungaji bora kwa ligi za Ulaya nzima ni kutokana na kuhusisha wakali wote matata katika kuweka mipira kambani.

Messi anaongoza kwa sasa akiwa na ameweka kambani mabao 21 huko kwenye La Liga na kila bao moja lina thamani ya pointi mbili, kwa Ligi Kuu tano bora za Ulaya, ikiwa ni La Liga, Ligi Kuu England, Bundesliga, Ligue 1 na Serie A. Kutokana na hilo, hivyo Messi atakuwa na pointi 42 kwenye mchekamchaka wa kuwania ufungaji bora wa Ulaya.

Kylian Mbappe na Ronaldo wanafuatia, kutokana na kila mmoja kufunga mabao 18 kwenye Ligue 1 na Serie A mtawalia na hivyo kuwa na pointi 36 kila mmoja. Kisha anakuja Edinson Cavani, aliyefunga mabao 17 kwenye Ligue 1 sawa na Sergio Aguero na Mohamed Salah walivyofanya huko kwenye Ligi Kuu England na hivyo kuwa na pointi 34 katika mbio hizo.

Fabio Quagliarella wa Sampdoria na Duvan Zapata wa Atalanta wao kila mmoja amefunga mabao 16 kwenye Serie A na hivyo kujikusanyia pointi 32, wakati Nicolas Pepe wa Lille naye ametupia mara 16 kwenye Ligue 1 na kuwa na pointi 32 sawa na kina Zapata. Luis Suarez na Pierre-Emerick Aubameyang wapo nyuma huko na mabao yao 15 kila mmoja na hivyo kujikuta wakiwa wamekusanya pointi 30 tu katika mbio hizo za kusaka kiatu cha Ulaya. Wachambuzi wa mambo ya soka wanaamini licha ya ushindani kuwa ni mkubwa, lakini mastaa Messi, Ronaldo na Mbappe ndio watakaotoana jasho mwanzo mwisho kwenye kuisaka tuzo hiyo binafsi kwa mchezaji mwishoni mwa msimu huu.

TOP SIX MSIMAMO WA MABAO

1.Messi - mabao 21, pointi 42

2.Mbappe - mabao 18, pointi 36

3.Ronaldo - mabao 18, poionti 36

4.Cavani - mabao 17, pointi 34

5.Aguero - mabao 17, pointi 34

6.Salah - mabao 17, pointi 34.