Kasi ya Geita Gold yawapa presha wapinzani

Saturday February 9 2019

 

By MASOUD MASASI

GEITA Gold FC ndio inayoongoza Ligi Daraja la Kwanza Kundi B ikiwa na pointi 26 lakini Kocha wa Pamba FC, Ally Kisaka amesema hakuna kingine cha kukimbizana na timu hiyo zaidi ya kuifunga Transit Camp leo Jumamosi katika Uwanja wa Nyamagana jijini Mwanza.

Mpaka sasa Pamba FC yenye maskani yake jijini hapa ina pointi 20 ikishika nafasi ya nne kwenye msimamo wa Kundi B.

Kisaka alisema kwasasa kila mchezo kwake ni kama fainali kwani wanataka kushinda ili kuendana na kasi ya Geita Gold ambayo inayoongoza kundi ikiwa na pointi 26.

Alisema kikosi chake kipo fiti kuelekea mchezo huo na pointi tatu ndizo zitakazoifanya ipate nguvu za kupambana kwenye ligi hiyo.

“Tunahitaji ushindi ingawaje hatuwafahamu wapinzani wetu, ila tukishinda tutakuwa na pointi 23 zitatufanya tuwe nafasi nzuri ya kupambana na Geita Gold, hivyo ushindi ni muhimu,” alisema Kisaka.

Kocha huyo aliwataka mashabiki wa Pamba kufika kwa wingi kutoa sapoti kwa wachezaji wao na uwepo wao utasaidia kupata matokeo mazuri.

“Mashabiki tunahitaji sapoti yao kwenye huu mchezo ambao utatupa nguvu kubwa ya kuendelea kupambana kwenye ligi iwapo tutashinda,”alisema kocha huyo.

Advertisement