Kashindikana

Muktasari:

Hapo wachambuzi wa soka wakaanza kuchonga kama kawaida, ambapo akatakiwa kufuata staili kama za Tonny Pullis aliyekuwa na Stoke City ama Big Sam.

Manchester,England.Manchester City ndio ishajibebea ubingwa wake wa Ligi Kuu England kwa mara ya pili mfululizo ikiwa chini ya Mhispaniola, Pep Guardiola.

Kwa sasa mashabiki wa Man City wanarusha vijembe tu kwa wenzao wa Manchester United, ambao msimu huu wameendelea kuwa wanyonge kwani chama lao linachapwa tu nje ndani.

Lakini, gumzo kubwa kwa sasa ni uchawi wa Guardiola, ambaye suala la kubeba mataji makubwa s si jambo la ajabu sana kwani ameshafanya vizuri katika klabu kubwa tatu.

Ameshabeba mataji ya La Liga akiwa na Barcelona kisha akaenda zake Bundesliga nako akabeba mataji akiwa na Bayern Munich. Swali kubwa ambalo dunia inajiuliza kwa sasa ni kama Guardiola atarudia ubabe wake wa kubeba taji hilo mara tatu kama alivyofanya alipotoka.

Hata hivyo, wakati anatua England kuanza kibarua chake akakutana na Leicester City ambao ndio walikuwa wanamiliki taji hilo. Katika mechi zake za awali, mambo hayakuonekana kuwa mazuri kwa Pep.

Hapo wachambuzi wa soka wakaanza kuchonga kama kawaida, ambapo akatakiwa kufuata staili kama za Tonny Pullis aliyekuwa na Stoke City ama Big Sam.

“Amekuwa hapa kwa miezi minne hakuna anachofanya. Ni kama soka letu linamkataa tu na staili zake za La Liga ama Bundesliga ni kama haziwezi kumfanya akaendelea kuwa kocha bora hapa England.”

Msimu wa 2016 ulianza vizuri tu, lakini walipopata kichapo cha 4-1 kutoka kwa Leicester City ndipo kiwango cha ufundishaji cha Guadiola kilipoanza kubezwa. Katika moja ya majadiliano na waandshi wa habari alisema; “Ligi hii watu wanatumia nguvu sana, sipo hapa kufundisha timu ili ikwatue watu. Nataka kufundisha timu kucheza vizuri kistaarabu na kuanza kufunga mabao.”

Baada ya kauli hiyo, wachambuzi wa soka walimvamia na kumchambua kwamba, ameshindwa rasmi soka la Uingereza. ìHivi huyu kocha anafikiri England ni pa kuchezea eeh! Yaani anadhani kuna watu watakuwa wanampa pasi nzuri ili aendeleza mbwembwe kwa dakika 90,”

Lakini, sasa watu hao wanasema nini? Pep alianza kwa kuhangaika na kama si uvumilivu wa mabosi wake huenda wangemtimua. Lakini, baada ya kukipanga kikosi chake ndipo akarudi na nguvu mpya, ambayo matokeo yake yameendelea mpaka msimu huu ulipomalizika.

Kwanza alikubali yupo katika ligi ya kutumia nguvu, hicho kisingeweza kubadilika, Pep aliamua kutafuta namna ya kupenya katikati ya msitu wa mbinu za England.

Mwisho wa dharau

Agosti 12, 2017, ilikuwa ni msimu wa pili kwa Guardiola kuinoa Manchester City. Bado watu walikuwa na wasiwasi, hawakuona kama anaweza kupindua meza. Walishinda mchezo wa kwanza dhidi ya Brighton kwa mabao 2-0 huo ukawa mwanzo wa ushindi mwingi tu. Waliendelea kufanya kweli. Katika kipindi cha msimu miwili wamepata pointi 198 na hizo zilitosha kuwapa vikombe viwili. Na katika wakati huo kikosi kimetikisa nyavu zaidi ya mara 200.

Akizungumza baada ya kubeba ubingwa huo kwa mara ya pili, Guardiola alisema; ìNimekuja Ligi Kuu England kujaribu kupata mafanikio baada kufanya hivyo kule La Liga na Bundesliga.

“Kule Ujerumani, walidhani nitashindwa sababu ya staili yangu ya kumiliki mpira, lakini, nilitwaa mataji matatu. Unatakiwa kubadili staili unapokuwa kwingine ila ushindi.”