Kashasha: Yanga walikwama hapa…

Muktasari:

Simba itashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku mshindi wa fainali za Kombe la Shirikisho atashiriki michuano ya kimataifa ya Kombe hilo barani Afrika.

JANA Jumapili, Yanga walipokea kipigo cha mabao 4-1 dhidi ya Simba katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Azam (ASFC), matokeo ambayo mchambuzi maarufu nchini Alex Kashasha amesema ni kama Yanga walijitakia.

Kwa matokeo hayo, Yanga sasa hawatashiriki michuano yoyote ya kimataifa kwani tayari ubingwa wa Ligi Kuu Bara umechukuliwa na Simba ambao wametinga hatua ya fainali ya michuano hiyo itakayochezwa Agosti 2 mjini Sumbawanga dhidi ya Namungo FC.

Simba itashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika huku mshindi wa fainali za Kombe la Shirikisho atashiriki michuano ya kimataifa ya Kombe hilo barani Afrika.

Namungo sasa ni kama hana cha kupoteza kwani hata wasipotwaa ubingwa huo wamepata nafasi ya kushiriki michuano hiyo kwani kama Simba atatwaa kombe hilo hawezi kushiriki kutokana na kanuni ilivyo maana tayari imepata uwakilishi kimataifa.

Kashasha amesema maandalizi ya kufanya vizuri katika msimu husika huwa yanaonekana mwanzo wa msimu katika (Pre Season), na kwamba Simba walijiandaa vizuri ndio maana wanapata mafanikio mengi msimu huu wakati Yanga wao walifanya maandalizi ya kiujanja ujanja.

Amesema jambo lingine ambalo limechangia Yanga kutofanya vizuri katika mechi ya Simba ni usajili wa kawaida mno wa  wachezaji ambao huwezi kwenda kuwalinganisha na ambao wanapatikana kikosi cha mabingwa hao ndio maana walizidiwa.

"Katika mechi yenyewe kocha wa Yanga, Luc Eymael alifanya makosa kwenye kikosi chake ambacho alikianzisha kwani kulikuwa na wachezaji zaidi ya wanne uwezo wao ulikuwa chini ila walicheza kutokana na ukubwa wa majina.

"Wachezaji wengi wa Yanga walionesha udhaifu pindi timu ilipokuwa inashambulia na hata pale ilipokuwa inashambuliwa walikuwa hawafanyi kazi ya kuwakaba wachezaji wa timu pinzani ambao walikuwa wakicheza kwa kujiachia mno," amesema.

"Wakati wachezaji wa Yanga wakionesha madhaifu hayo kwenye kukaba na kushambulia kwa wapinzani wao Simba mambo yalikuwa ni tofauti kwani wachezaji wao wengi walikuwa imara na walicheza vyema idara zote tatu ulinzi, kiungo na ushambuliaji.

"Nguvu ya Simba ilikuwa inapatikana eneo la kiungo waliocheza katikati na pembeni ambao walikamata mechi na kutoa mchango mkubwa kwa timu yao kuibuka na ushindi huo ambao kama wangeongeza umakini zaidi wangepata mabao zaidi ya hayo," amesema Kashasha.