Kaseja mfano wa kuigwa Afrika Mashariki

Muktasari:

Nashukuru kwamba Kaseja tulifanya naye kazi safi sana pale Jangwani. Wengi sana waliocheza na Kaseja wamestaafu soka.

KAMA kuna mchezaji ambaye kwa kweli anafaa kuigwa na wanaokipiga sasa hivi katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki na Kati si mwingine, bali ni mlinda lango Juma Kaseka wa timu ya soka ya KMC iliyopo Tanzania.

Nashukuru Mungu kwamba ni mchezaji ambaye tulipiga naye kazi pale Mtaa wa Jangwani wakati nakipiga katika Klabu ya Yanga. Huyu ni mojawapo wa wachezaji ambao nawavulia kofia kwa heshima zake.

Ni mojawapo wa wachezaji wenye nidhamu ya juu kabisa katika soka la kanda hii. Historia tayari inakuonyesha kwamba ni mchezaji ambaye amecheza Ligi Kuu Tanzania Bara kwa miongo miwili sasa. Amekipiga kwa miaka 20 sasa, kama sijakosea.

Kumbuka alianza soka na Moro United katika Ligi Kuu ya Tanzania kabla ya kujiunga na Klabu ya Simba misimu mitatu baadaye.

Mimi mwenyewe nimekuja kukutana naye Yanga msimu wa 2008/09 na tuliweza kunyakua taji msimu huo akiwa mojawapo wa walinda lango Mtaa wa Jangwani, akiwa na Obren Curkovic, bila kumsahau Ivo Mapunda na Steve Marashi.

Jambo la muhimu sana ambalo nitalizingumzia leo ni nidhamu. Katika masuala yako yote ya maisha lazima uwe na nidhamu.

Pasipo kuwa na nidhamu, ndugu zanguni sidhani kama kazi itafanyika vilivyo.

Nashukuru kwamba Kaseja tulifanya naye kazi safi sana pale Jangwani. Wengi sana waliocheza na Kaseja wamestaafu soka.

Kwa hiyo kufikia hatua hii ya kukipiga kwa zaidi ya miaka 20 Ligi Kuu Tanzania si mchezo ndugu zanguni. Inahitaji nidhamu ya hali ya juu.

Kaseja kwa kweli amejiweka vizuri sana. Hakuna siku ambayo niliwahi kusikia au kumuona katika midundo ya huku na kule. Alizingatia kazi yake vilivyo. Aliheshimu kazi yake. Alikuwa anajifua kweli kweli katika mazoezi pale Jangwani. Hakupenda kufungwa. Angefoka wakati timu yake inafungwa mazoezini.

Ni baadhi tu ya wachezaji wachache walikuwa wanafahamu nini kiliwaleta Jangwani. Nakumbuka kuna nyakati zingine tulikuwa tunabaki na yeye uwanjani kupiga mazoezi ya ziada. Alikuwa anapenda kujipa kazi ya ziada. Ushupavu wake ulitokana na kujiheshimu.

Kaseja alijiunga na Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2000 akitokea Moro United. Hatimaye akatimkia klabu ya Simba msimu wa 2003. Ule msimu wa 2008/09 akajiunga na Yanga, lakini 2009/10 akarejea Simba hadi 2013. Msimu wa 2014 akarejea Yanga tena.

Huko hakukaa sana baadaye akaondoka akaelekea Mbeya City msimu wa 2015/16. Msimu wa 2017 akakipiga pale Kagera Sugar. Kwa Sasa yupo katika kikosi cha KMC jijini Dar es Salaam.

Jambo la kufurahisha ni kwamba viwango vya Kaseja havijawahi kushuka hata kidogo. Heshima yake ni lazima tumpe.

Inanifurahisha kuona kwamba yupo katika kikosi cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, jambo ambalo linafaa kuigwa na wachezaji wa kanda hii.

Kuchaguliwa kuwa katika kikosi cha timu ya Taifa kama mlinda lango nambari moja, na umri wake inaonyesha kwamba bila nidhamu hauwezi kwenda mbali kimaisha.

Kaseja ni mojawapo wa walinda lango wazuri kwa kuokoa mikwaju ya penalti. Lakini hata hivyo najivunia kuwa mchezaji pekee Yanga ambaye Kaseja hakuwahi kuokoa penalti yangu. Hahahahaaaa!

Kaseja ni kipa ambaye hauwezi kupiga penalti tano ashindwe kudaka hata moja. ni mzuri sana. Lakini nabaki na hizo sifa za kumtungua zote tano. Hatari huyu Kaseja.

Huyu ni mfano ambao unafaa kuingwa katika kanda hii kwa wachezaji wetu.

Ni wazi kwamba sidhani kama kuna mchezaji katika ukanda huu ambaye amecheza muda huo mrefu isipokuwa Juma Kaseja. Juzi katika mechi ya kimataifa alionyesha ujasiri wake wote na ni wakati wake kuheshimiwa.

Mashabiki wengi wamekuwa wakiwaona wachezaji. Haimaanishi ukitoka Yanga, Simba, AFC Leopards, Gor Mahia na kadhalika kiwango chako kimaisha kinakwisha. La hasha.

Kwa hiyo ni lazima tuzowee kuwaheshimu wachezaji ambao wametusaidia kwa njia moja ama nyingine. Kaseja ametwaa mataji matano ya Ligi Kuu Tanzania Bara akiwa na Simba, na taji moja akiwa na Yanga.

Heshima lazima idumu ndugu zanguni. Mnyonge mnyongeni lakini heshima yake mpeni. Wakati Kaseja akiamua kustaafu ni lazima Watanzania wamkumbuke sana.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) ni lazima limwandalie mechi ya kustaafu. Lini? Haijulikani kwa Sababu ndugu yangu bado yupo kikazi na nguvu na uwezo wa kuzidi kupiga shughuli uwanjani.

Mchezaji mwingine pia anayeelekeana na Kaseja hapo ni Mrisho Ngasa. Heshima zake apewe pia. Nawatakia kila la heri.

Kariba ya wachezaji wa aina hii akiwamo na ndugu Erasto Nyoni ni watu wa kuheshimiwa katika soka la Bongo. Huyu naye ana muda mrefu pale Taifa Stars ambako mpaka leo bado anapambana na vijana na anaipa mafanikio timu yao kwenye medani ya mchezo wa soka.

Hawa ni wazaleondo halisi wa Bongo.