Kaseja apania makubwa fainali za Mataifa ya Afrika

Muktasari:

Kaseja tumejipanga kwaajili ya kushindana na sio kushindwa tumeondoka tukiwa tumejiandaa hatuendi nchi za watu kwaajili ya kutalii tumefanya vizuri nyumbani na ugenini tunategemea kufanya ivyo.

Dar es Salaam. Nahodha wa timu ya Taifa ya Tanzania ya Soka la Ufukweni, Juma Kaseja amesema uwezo makocha wao Boniface Pawasa na Talib Hilal utawasaidia kufanya vizuri katika mashindano ya Mataifa ya Afrika kwa Soka la ufukweni nchini Misri zinazotarajia kuanza Desemba 8 mpaka14, 2018.

Kaseja alisema wachezaji wengi walioitwa ni wale wenye uzoefu na soka la ufukweni na wamekuwa wakifanya vizuri kwenye michuano ya ndani ikiwemo yale mashindano ya Copa Dar es salaam ambayo yamemalizika hivi karibuni kwa Tanzania kuibuka bingwa mbele ya nchi za Malawi, Uganda na Shelisheli.

Kaseja aliweka wazi kuwa wapo Kundi B ni gumu lenye timu za Senegal, Nigeria na Libya, lakini kwenye mchezo wa soka lolote linawezekana na wao wamejipanga kushinda kama ilivyo kwa timu nyingine hivyo hawahofii wapinzani wao.

Kikosi cha timu hiyo kimeondoka kikiwa na nyota 12, pamoja na Ibrahim Abdallah, Juma Ibrahim, Rolland  Msonjo, Samwel Mauru, Yahya Tumbo, Jaruph Juma, Ahmad  Ahmad, Alfa Tindise, Kashiru Said, Mohamed Makame, Juma Kaseja na Mbwana Mussa.