TASWIRA YA MLANGABOY : Karibu Ndayiragije, piga kazi tuachie yetu wenyewe

Muktasari:

Mrundi Ndayiragije amepewa jukumu hilo la muda na TFF na atasaidiwa na kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda pamoja Selemani Matola ambaye ni kocha wa Polisi Tanzania.

Karibu Etienne Ndayiragije, karibu Tanzania, karibu sana Ndayiragije na pole na majukumu yako mapya.

Najua msomaji wangu utakuwa unajiuliza kwani leo ndiyo nakumbuka kumkaribisha wakati yupo Tanzania kwa zaidi ya miaka mwili sasa.

Kocha Ndayiragije aliwahi kuzinoa klabu za Mbao, KMC na sasa Azam FC, lakini hivi karibuni Shirikisho la Soka la Tanzania (TFF) limempa jukumu la kuiongoza timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ kwa muda katika michezo ya kusaka tiketi ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ndani (CHAN2020) nchini Cameroon.

Tanzania itacheza mechi ya kwanza dhidi ya Kenya hapo Julai 28 na kurudiana huko Nairobi, Agosti 4.

Na endapo Stars itafanikiwa kushinda mchezo huo, basi itacheza na mshindi wa mechi kati ya Burundi na Sudan Kusini kusaka nafasi ya kufuzu kwa fainali hizo zitakazofanyika Cameroon kati ya Januari na Februari 2020.

Mrundi Ndayiragije amepewa jukumu hilo la muda na TFF na atasaidiwa na kocha wa Coastal Union, Juma Mgunda pamoja Selemani Matola ambaye ni kocha wa Polisi Tanzania.

Nimeanza kwa kumkaribisha kwa bashasha Ndayiragije katika jukumu hilo jipya japokuwa ni jambo la muda tu, ila naamini katika kipindi hiki kifupi atawajua vizuri Watanzania.

Wiki hii ametangaza kikosi chake kwa ajili ya mchezo dhidi ya Kenya kwa kuangalia haraka nimeona Ndayiragije na wasaidizi wake wamejaribu kujiondoa katika lawama kwa kuita nyota wa kuwafurahisha wadau wa soka.

Makipa: Juma Kaseja (KMC), Aishi Manura (Simba), Metacha Mnata (Yanga).

Mabeki: Paul Godfrey (Yanga), Boniface Maganga (KMC), Gadiel Michael (Simba), Paul Ngalema (Namungo), David Mwandika (Azam), Idd Mobi (Polisi Tanzania), Kelvin Yondani (Yanga), Erasto Nyoni (Simba).

Viungo: Jonas Mkude (Simba), Abdulazizi Makame (Yanga), Mudathil Yahya (Azam), Ibrahim Ajibu (Simba), Salum Aboubakari (Azam), Feisal Salum (Yanga), Frank Domayo (Azam), Hassan Dilunga (Simba).

Washambuliaji: John Bocco (Simba), Salum Aiyee (KMC), Iddy Nado (Azam), Ayuob Lyanga (Coastal Union), Kelvin John (U-17) na Shabani Chilunda (Azam).

Ndayiragije amekwepa kelele na mashambulizi aliyoyapata Emmanuel Amunike baada ya kuwarudisha kundini Ibrahimu Ajibu, Jonas Mkude, Salum Aboubakari ‘Sure Boy’ kwa ajili ya mchezo dhidi ya Kenya.

Ukiangalia sehemu kubwa ya lawama kwa Amunike zilianza baada ya kuwaacha nyota hawa watatu ambao wale wadau wanaamini ni viungo bora waliostahili kwenda Misri.

Mrundi huyo amesikia kilio cha wadau kwa kumuita kwa mara ya kwanza aliyekuwa mfungaji bora wa pili wa Ligi Kuu Bara, Salum Aiyee wa KMC ambaye msimu uliopita alifunga mabao 18 katika ligi akiwa na Mwadui FC.

Mrundi huyo amewajumuisha kiungo mpya wa Yanga, Abdulaziz Makame pamoja na beki chipukizi Paul Godfrey, chipukizi Kelvin John pamoja na kipa mkongwe Juma Kaseja ameitwa katika kikosi hicho cha wachezaji 25.

Kwa kufanya hivyo Ndayiragije ametufunga midogo kwa muda hatuna pa kumlaumu kwani kila tuliyetamani awepo Stars ameitwa.

Ila ajiande kisaikolojia iwapo Tanzania itafungwa na Kenya katika mchezo wa kwanza, basi atapokea kila aina ya lugha mbaya kutoka kila kona ya nchi kuanzia kwa mwanafunzi, waandishi, wachambuzi, wanasiasa hadi viongozi wakubwa wa serikalini.

Naomba ajiandaye kuvumia zaidi kwa sababu wakati ule Mbao alipigwa zengwe kidogo tu na watu wachache wa Mwanza aliikimbia timu.

Ukiwa kocha wa Taifa Stars haijalishi ni kocha wa kudumu au muda ni lazima ujiandae kupokea lugha za kuudhi hasa unapokataa kuwapanga wachezaji ambao wewe kocha unaona hawa ndio wanaofuata maelekezo na kukidhi vigezo vyako.

Watanzania ni wazuri wa kuwalaumu makocha na kuwashushia shutuma kwamba uwezo wao mdogo na hawana hadhi ya kufundisha timu yao ya taifa.

Tumewaona makocha wakubwa wa viwango mbalimbali wakitukanwa na kudhalilishwa na wadau wa soka, kisa tu kufanya vibaya kwa Stars na hasa kwa kuwa wamewaacha wale wachezaji wanaoamini wao kuwa ni bora.

Kwa hiyo Ndayiragije ni lazima alijue hilo mapema, ameamua kuchukua jukumu hili ni zuri kwa CV yake, lakini asipojiandaa vizuri anaweza kuweka shakani hata kibarua chake cha Azam.

Watanzania ni wazuri wa kucheza mpira mdomoni na kuona makosa ya makocha, pia ni mabingwa wa kutoa mbinu za mdomoni, lakini wameshindwa kuwasaidia wachezaji wachezaji wetu kujitambua hasa inapofika katika kuchezea timu ya taifa.

Karibu sana Ndayiragije nakutakia mafanikio mema katika kibarua chako cha muda ila sisi Watanzania tunacheza mpira mdomoni.

Unapoianza kazi yako ni vyema zaidi ikajiandaa kwa kila zuri na baya, lakini kwetu Wabongo, lawama ni kitu cha kwanza.